Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT-TAIFA), Sheikh Dkt.Alhad Mussa Salum, ametoa ufafanuzi Maridhawa kuhusu mambo ya mitume na manabii kwamba hayatakiwi kuwakwaza watu wengine. Kwamba tutakaposikia fulani wanamuita mtume au nabii, hakuna haja ya wewe kukerekwa ikiwa hilo sio kwa mujibu wa Imani yako, kwa maana litakuwa halikuhusu, sasa kwani lisilokuhusu uonyeshe linakuhusu?!.
Aisha, Dkt. Alhad Mussa Salum aliendelea kubainisha na kufafanua zaidi akisema:
Kwa mfano: Sisi Waislamu, tutakaposikia watu wanajiita au wanaitwa mitume na manabii kwa mujibu wa vitabu vyao, sisi Waislamu inatuhusu nini?!.
Sisi kama Waislamu, Imani yetu hakuna mtume wala nabii baada ya Mtume (Nabii) Muhammad (saww). Hiyo ndio Imani yetu Waislamu.
Sasa, wakati wengine wasiokuwa Waislamu wanapojiita au kuitwa manabii na mitume kwa mujibu wa vitabu vyao wao, Sisi wengine hilo litakuwa linatuhusu nini?! Kwanini tukereketwe na jambo lisilotuhusu?!.
Na sisi tukiwaita mitume au manabii, hatuwaiti hivyo kwa Imani zetu kama Waislamu, bali ni kwa mujibu wa Imani zao.
Na Quran Tukufu inasema:
"Mwenyezi Mungu hatizami sura zenu wala miili yenu, bali anatizama ndani ya mioyo yenu".
Hiyo ndio Quran inavyosema na kutuelekeza.
Udugu wa Watanzania:
Sisi tunatakiwa kuzingatia udugu wetu. Sisi sote ni ndugu katika nchi yetu.
1_Tuna udugu wa kiinchi kama Watanzania.
2_Lakini pia tuna udugu wa Kibinadamu, sisi sote ni Watoto wa Adam (as).
3_Na kuna udugu wa Kidini, kwamba Wakristo wakiwa kanisani kwao, wao kwa wao ni ndugu Kidini, na Waislamu pia wakiwa Msikitini kwao, ni ndugu wao kwa wao, kisha wote kwa pamoja tunakuja kuunganishwa na udugu wa Kibinadamu na kiinchi.
Amani ya Watanzania:
Hivyo, udugu huu unatufanya kuishi kwa pamoja kwa Amani na Maridhiano katika nchi yetu.
Mafunzo ya Dini ya Uislamu na Ukristo, yanasisitiza na kulingania Amani. Hakuna Dini inayofundisha kutokuwa na Amani, ukatili dhidi ya mtu mwingine.
Kuheshimiana kama Watanzania:
Kila mtu anatakiwa kusoma Imani ya mwenzake. Ukijua huyu Imani yake ni hii, huwezi kumbughudhi kwa sababu hiyo ndio imani yake, na utamheshimu kwa Imani yake naye pia atakuheshimu kwa Imani yako.
Uislamu unatufunza kuwa Muislamu wa kweli ni yule ambaye atawasalimisha watu na ulimi wake na mkono wake. Hakuna Muislamu anamdhulumu mtu kwa sababu ya tofauti ya kiimani, huyo hatokuwa Mfuasi Sahihi wa Uislamu.
Makusudio ya Sheria hapa Duniani ni:
1_Kuhifadhi Nafsi. Kila mtu alindwe na kuhufadhiwa Nafsi yake.
2_Kuhifadhi Akili. Sheria inataka Akili ilindwe na kuhifadhiwa. Ndio maana inaharamishwa Bangi, madawa ya kulevya, pombe na vilevi vya kuharibu Akili ya Mwanadamu.
3_Kuhifadhi Kizazi, nasaba. Kizazi lazima kilindwe na hili ndio kusudio la Sheria.Ndio maana kuna Ndoa, kuoana Mume na Mke. Ajulikane mama, Baba, mjomba, Shangazi n.k namna hiyo Kizazi kinahifadhiwa.
4_Kuhifadhi Mali. Mali ni lazima ihifadhiwe. Ni kosa kuharibu Mali ya mtu. Hata kuitumia hivyo ni haram Sheria haikubali.
5_Kulinda Dini. Dini lazima ilindwe. Na kama unataka mtu aingie katika Dini yako ni utumie maneno mazuri ya Hekima, bila kumbughudhi.
6-Kulinda nchi. Nchi lazima ilindwe na kuhifadhiwa.
Jumuiya ya Maridhiano na Amani inatambua umuhimu wa kulinda nchi, na ndio maana inashirikiana na Serikali kulinda Amani. Amani lazima ilindwe na kuhifadhiwa. Hasa katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu unaokuja, Amani inatakiwa kulindwa na kila awe na Amani kuchagua Kiongozi wake kwa Amani.
Ubaya wa Rushwa katika nchi:
Pia rushwa ni jambo baya, mtoa rushwa na mpokea rushwa, wote ni wabaya na wote motoni.
Ni kama vile shoga na basha, wote wabaya. Na mabasha ni wabaya zaidi kuliko hata mashoga.
Azma ya Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania:
Kiujumla, azma ya Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania ni kusimama bega kwa bega na Serikali katika kulinda na kudumisha Amani ya na Maridhiano ya nchi yetu kwa ajili ya Ustawi wa nchi yetu.
Sheikh Dkt.Alhad Mussa Salum - Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT-TAIFA)
Your Comment