Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Televisheni ya Kizayuni Channel 7 leo imefichua kuwa jeshi la Israel, kutokana na upungufu mkubwa wa wanajeshi, linafikiria kuajiri Wayahudi kutoka mataifa ya kigeni kwa kuwahamasisha wahamie katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kujiunga na jeshi kwa masharti ya kulipwa mishahara mikubwa.
Vyanzo vya Kizayuni vimefichua kuwa jeshi la Israel limeamua kutumia mbinu hii mpya ili kukabiliana na ukosefu wa askari wa mstari wa mbele na askari wa akiba, huku serikali ya Kizayuni ikiwa tayari imepanga kuikalia kikamilifu mji wa Gaza.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa uhaba wa wanajeshi wa Israel unakadiriwa kufikia kati ya askari 10,000 hadi 12,000. Upungufu huu unatokana hasa na kukataa kwa makundi ya Haredi (Wayahudi waorthodox wenye misimamo mikali) kutuma vijana wao jeshini, jambo lililoibua mgogoro wa ndani kuhusu sheria ya ajira ya lazima jeshini.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jeshi la Israel linapanga kuwalenga zaidi Wayahudi vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 25 kutoka Marekani na Ufaransa, kuwahimiza wahamie katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kujiandikisha jeshini kwa kipindi cha miaka kadhaa.
Takwimu zinaonyesha kuwa jeshi la Israel lina uwezo wa kupokea wanajeshi 10,000 wa kigeni kila mwaka, lakini kwa sasa limeweka lengo la awali la kuajiri vijana 600 hadi 700 pekee kila mwaka.
Maafisa wa kijeshi na usalama wamesema mpango huu bado uko katika hatua za awali za maandalizi, lakini wanatarajia utasaidia kujaza mapengo yaliyopo kwa kuibua hisia za "kizalendo" miongoni mwa Wayahudi waishio ughaibuni.
Ripoti pia imesisitiza kuwa karibu miaka miwili tangu kuanza kwa vita vya Gaza, jeshi la Israel linakabiliwa na upungufu mkubwa wa wanajeshi na askari wa akiba, pamoja na uchakavu wa vifaa vya kivita, hali inayolifanya lijikute kwenye changamoto kubwa zaidi.
Wakati huo huo, baraza la mawaziri la Kizayuni limeamua kupanua vita kwa lengo la kuikalia kikamilifu Gaza, likilenga zaidi kuhifadhi mamlaka yake ya kisiasa ndani ya Israel.
Your Comment