25 Agosti 2025 - 22:27
Abu Muhammad al-Jolani Kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Huku Akiwa Chini ya Vikwazo

Ahmad al-Sharaa, maarufu kama Abu Muhammad al-Jolani, Rais wa Serikali ya Muda ya Syria, anatarajiwa kushiriki na kutoa hotuba katika kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York katika wiki chache zijazo.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kwa mujibu wa taarifa ya afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria aliyoeleza kwa Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), Jolani atahutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Al-Sharaa atakuwa rais wa kwanza wa Syria tangu mwaka 1967 kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, na vilevile ni mara ya kwanza kwa rais wa Serikali ya Muda ya Syria kushiriki katika wiki ya viongozi wakuu wa kikao hicho kitakachofanyika kuanzia Septemba 22 hadi 30.

Serikali ya muda ya Syria chini ya uongozi wake, tangu ilipochukua madaraka mjini Damascus mnamo Desemba 8 iliyopita, imekuwa ikipata uungaji mkono wa kikanda na kimataifa. Hata hivyo, Ahmad al-Sharaa maarufu kama Jolani, bado yupo chini ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa kutokana na historia yake ya kigaidi, na kwa safari yoyote ya nje hulazimika kupata kibali maalum.

Awali, mnamo Aprili 25, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Jolani, Asaad al-Shaybani, kwa mara ya kwanza alihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati bendera ya serikali ya Jolani ikipandishwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York sambamba na bendera za nchi wanachama 192.

Aidha, mnamo Mei 14, Ahmad al-Sharaa maarufu kama Abu Muhammad al-Jolani alikutana na Rais wa Marekani Donald Trump nchini Saudi Arabia, mkutano uliokuja siku chache baada ya ziara yake mjini Paris ambapo alikutana na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha