9 Septemba 2025 - 14:42
Mtume Mtukufu (s.a.w.w) na Sanaa ya Kuonyesha Mapenzi Ndani ya Familia

Familia katika mtazamo wa Mtume Mtukufu (s.a.w) si tu kitovu cha utulivu, bali ni uwanja wa kudhihirika kwa maadili ya kimungu. Yeye (s.a.w.w), kwa tabia yake tukufu na kwa kushikamana na mafundisho ya Qur'an kama vile: " - Semeni naye - kwa upole" (قَوْلًا لَّیِّنًا), na "Hakika wewe ni mwenye tabia njema kabisa" (إِنَّکَ لَعَلَىٰ خُلُقٍ عَظِیمٍ), alionesha ustadi wa kipekee katika kuonyesha mapenzi kwa wake na watoto wake. Makala hii, ikitegemea vyanzo vya Kishia, inachunguza mwonekano wa upendo wa Mtume (s.a.w.w) ndani ya familia, na inatoa mafunzo ya kudumu kwa familia za leo.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-: Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Hussein Amin, ambaye ni mwandishi na mtafiti wa masuala ya dini, katika makala maalum aliyoandika kwa ajili ya ABNA, amezungumzia kuhusu “sanaa ya kuonyesha mapenzi ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w) ndani ya familia.”

Kwa kutegemea Aya za Qur’an Tukufu na sira (maisha na mwenendo) ya Mtume (s.a.w.w), ameuchambua kwa kina muktadha wa kimaadili na kihisia wa tabia ya Mtume (s.a.w.w) katika mazingira ya kifamilia.

Mtume Mtukufu (s.a.w.w) na Sanaa ya Kuonyesha Mapenzi Ndani ya Familia

Mtume Mtukufu (s.a.w.) na Sanaa ya Kuonyesha Mapenzi Ndani ya Familia

Muhammad Hussein Amin / Mwandishi na Mtafiti wa Masuala ya Dini

Maisha ya kifamilia ya Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w) yalikuwa taswira hai ya upendo, huruma, na mapenzi safi ya kimungu. Pamoja na cheo chake cha utume na majukumu yake makubwa ya kijamii, Mtume (s.a.w.w) hakupuuza hata fursa ndogo ya kuonesha mapenzi kwa familia yake.

Kwa mujibu wa Qur’an Tukufu na hadithi sahihi, mtazamo wa Kishia humtazama Mtume (s.a.w.w) kuwa si tu kama Kiongozi wa Umma, bali pia kama kielelezo bora cha mahusiano ya karibu na ya kiupendo katika familia. Kutokana na mtazamo huu, kujifunza sanaa ya kuonyesha mapenzi ya Mtume (s.a.w.w) ni nuru kwa familia za leo, ambazo zinatafuta utulivu katikati ya dhoruba za maisha ya kisasa.

Mapenzi Kwa Maneno: Lugha ya Upendo ya Mtume (s.a.w.w)

Mtume (s.a.w.w) mara kwa mara alitumia maneno matamu na yenye mapenzi kutuliza moyo wa familia yake. Alizungumza na wake zake kwa maneno ya heshima na huruma, akionyesha kwamba kusema maneno ya mapenzi si udhaifu, bali ni ukamilifu wa imani.

Qur’an Tukufu inasisitiza kusema kwa upole:

"Semeni naye kwa kauli laini" (Surat Taha: 44).
Na pia:
"Na hakika wewe una tabia njema kabisa" (Surat Qalam: 4).

Aya hizi mbili zinaonyesha wazi umuhimu wa tabia ya huruma na mawasiliano ya upendo katika familia.

Katika riwaya za Kishia, hasa kupitia Imam Swadiq (a.s), imeelezwa kuwa kuonyesha mapenzi kwa familia kuna thawabu kubwa na huleta mapenzi ya pande zote:

“Mwanamume anapomwambia mke wake: ‘Nakupenda,’ maneno hayo hayaondoki moyoni mwake milele.”

Mtume (s.a.w) alifanya kuonyesha mapenzi kuwa desturi, na hii ni nguzo ya maisha ya familia inayodumu. Maneno ya upendo yakitawala ndani ya nyumba, migogoro mingi huweza kumalizika.

Kushiriki Kazi za Nyumbani: Moyo wa Ushirikiano wa Mtume (s.a.w.w)

Mojawapo ya ishara bora za upendo wa Mtume kwa familia yake ni kushiriki kwake katika kazi za nyumbani. Licha ya nafasi yake ya juu, Mtume hakujiepusha na kazi. Alikuwa akishona nguo yake, kutengeneza viatu vyake, na kushiriki kazi kama wanaume wengine.

Katika hadithi imepokelewa:

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) alikuwa akishona nguo yake, kutengeneza kiatu chake, na kufanya kazi kama wanaume wengine ndani ya nyumba.”

Mtume (s.a.w.w) alifundisha kwa vitendo kuwa upendo si maneno tu, bali ni pia matendo. Familia zinazoshirikiana kwa moyo mmoja hukua zikiwa na mshikamano. Alivunja kiburi cha mfumo dume na kuwaalika wanaume kuwa washirika na wapenzi wa kweli wa familia zao.

Kuheshimu Heshima ya Mke: Misingi ya Heshima Katika Familia

Upendo wa Mtume (s.a.w.w) haukuishia kwa maneno ya mapenzi tu, bali pia alionyesha heshima ya kweli kwa wake zake. Alikuwa akiketi nao, kuzungumza nao kwa makini, na kuwasikiliza kwa uvumilivu.

Katika hadithi imepokelewa:

"Bora wenu ni yule aliye bora kwa familia yake, na mimi ni bora wenu kwa familia yangu."

Kauli hii inadhihirisha kuwa kipimo cha ubora wa mtu katika Uislamu si sura yake mbele ya jamii, bali ni mwenendo wake nyumbani.

Mtume (s.a.w) alionyesha kuwa mwanamke si mtumishi tu wa nyumbani, bali ni rafiki, mshauri, na mshirika wa kweli wa maisha. Mtazamo huu hujenga familia juu ya misingi ya heshima na mapenzi ya kweli.

Mapenzi Kwa Watoto: Kulea Kesho kwa Upendo

Mtume (s.a.w.w) aliwapenda sana watoto na wajukuu wake. Mara nyingi alikumbatia na kuwabusu Imam Hasan (a.s) na Imam Hussein (a.s). Imepokelewa kuwa alisema:

“Atakayembusu mwanawe, Mwenyezi Mungu atamwandikia thawabu; na atakayemfurahisha mwanawe, Mwenyezi Mungu atamfurahisha Siku ya Kiyama.”

Hili lilisemwa katika kipindi ambapo baadhi ya makabila waliona kumkumbatia mtoto kuwa udhaifu. Mtume (s.a.w) alivunja tamaduni hii mbaya na kutangaza kuwa kuonyesha mapenzi kwa mtoto ni thamani ya dini na maadili mema.

Mtume alionyesha kuwa mapenzi kwa watoto ni njia ya malezi ya kimungu inayokuza roho ya watoto wa baadaye kuwa viongozi bora wa jamii.

Kwa ujumla: Mtume (s.a.w.w) - Ni Kielelezo cha Familia ya Kiislamu

Sanaa ya Mtume (s.a.w.w) ya kuonyesha mapenzi katika familia ni mfano kamili kwa zama zote. Kuanzia kwenye maneno ya upendo hadi kwenye usaidizi wa kazi nyumbani, kutoka kwenye heshima kwa mke hadi upendo kwa watoto – yote yanaonyesha kuwa msingi wa familia katika Uislamu ni mapenzi na heshima.

Familia ya leo, ikiwa itafuata mwenendo wa Mtume (s.a.w.w), inaweza kusimama imara mbele ya changamoto za maisha ya kisasa na kufikia utulivu wa kweli.

📚 Vyanzo / Rejea:

  1. Qur’an Tukufu, Surah Taha, Aya ya 44.

  2. Qur’an Tukufu, Surah al-Qalam, Aya ya 4.

  3. Muhammad bin Hassan Al-Hurr Al-Amili, Wasa’il al-Shi’a, J. 20, Uk. 23.

  4. Allamah Majlisi, Bihar al-Anwar, J. 16, Uk. 207.

  5. Bihar al-Anwar, J. 71, Uk. 390.

  6. Muhammad bin Ya’qub Al-Kulayni, Al-Kafi, J. 6, Uk. 49.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha