9 Septemba 2025 - 18:24
Ayatollah Ramezani: Ueneaji wa Uislamu, zaidi ya kitu chochote, ulikuwa ni kwa sababu ya tabia njema ya Mtume (s.a.w.w)

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya AhlulBayt (a.s) akieleza kuwa tabia njema ya Mtume (s.a.w.w) ilikuwa ndiyo sababu kuu ya ushawishi wake, aliongeza: "Popote palipo na maadili ya Mtume, hakika yataacha athari yake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Ayatollah Reza Ramezani, katika sherehe ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu wa Uislamu, Muhammad Mustafa (s.a.w.w), na Imam Ja’far Sadiq (a.s), iliyofanyika katika jengo la Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s), alitoa pongezi kwa mnasaba wa kuwadia kwa Wiki ya Umoja na kumbukumbu ya kuzaliwa kwa viongozi hawa wawili wakuu wa Uislamu.

Aidha, alimshukuru Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kumuamini tena na kumteua kuendelea na jukumu lake ndani ya jumuiya hiyo, na akaeleza kuwa:

"Kuongoza na kuwatunza Mashia kote duniani ni jukumu kubwa na nyeti, ambalo limekabidhiwa kwa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s). Tunatumai kwamba kwa hatua mpya na mipango madhubuti, tutaweza kupiga hatua katika mageuzi na kuinua malengo makuu ya jumuiya."

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatollah Ramezani alisisitiza kuwa:

"Maadili si sawa na kulegeza misimamo. Wapo wanaodhani kuwa kuwa na maadili ni kule kujitoa au kutosema lolote mbele ya dhulma na uovu – lakini huu ni uelewa potofu."

Akinukuu aya ya 4 ya Suratul Qalam, inayosema kuwa:

"Na hakika wewe (Ewe Muhammad) uko juu ya tabia njema kabisa (khuluq ‘azim),"
alisema kuwa:
"Utukufu katika macho ya Mwanadamu una mipaka, lakini utukufu katika macho ya Mwenyezi Mungu hauna mipaka. Mtume (s.a.w.w) alifikia kilele cha maadili ambayo hatuwezi hata kuyaelewa."

Aliongeza kuwa:

"Kile kilichosambaza Uislamu si upanga wa Ali (a.s) wala utajiri wa Bibi Khadija (s.a), bali ni tabia njema ya Mtume (s.a.w.w). Kwa sababu huko Makka, kabla ya Hijra, hakukuwa na vita yoyote; Amri ya Jihad iliteremshwa baadaye akiwa Madina."

Ayatollah Ramadhani alifafanua zaidi:

"Tabia ya Mtume (s.a.w.w) ndiyo chanzo kikuu cha mvuto na ushawishi wake. Popote pale penye maadili ya Ki-Mtume, basi hakika pana athari njema."

Kisha alinukuu kauli ya Imam Ja’far Sadiq (a.s) aliyosema:

"Tunampenda mfuasi wetu (Shia) ambaye ni mwenye akili, uelewa, subira, adabu, ustahimilivu, na mkweli."

Akaendelea kusema:

"Jukumu la Jumuiya ni kutangaza mafundisho haya kwa dunia, na kuutambulisha uso halisi wa Ushia kwa msingi wa akili, roho (maadili), haki na wastani (msimamo wa kati)."

Pia alisisitiza kuwa:

"Mtu asiye na akili wala uelewa hawezi kuhesabiwa kuwa mfuasi halisi wa Ahlul-Bayt (a.s). Mafundisho ya AhlulBayt yanapaswa kufikishwa kwa wasomi na pia kwa watu wa kawaida kwa njia ambayo huimarisha uelewa wa kiakili."

Aliendelea kusema:

"Mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s) hutufundisha kupenda kwa wengine yale tunayopenda kwa nafsi zetu, na kuwachukia kwa wengine yale tunayoyachukia kwa nafsi zetu. Hii ndiyo ‘kanuni ya dhahabu’ ya maadili, ambayo inakubalika katika jamii yoyote au taifa lolote."

Akieleza kuhusu maadili ya mtu binafsi, alisema:

"Lazima tuanze kwa kujilea sisi wenyewe ili tufikie ushujaa, heshima ya ndani, utulivu, na matendo mema. Baada ya hapo, Mwenyezi Mungu atatuongoza katika mahusiano yetu na wengine."

Kisha akanukuu hadith ya Mtume (s.a.w.w):

"Yeyote anayenyenyekea, Mwenyezi Mungu atamwinua."

Akasisitiza kuwa:

"Lazima tuone kazi zetu kubwa kuwa ndogo, na kazi ndogo za wengine kuwa kubwa – kwa sababu ikhlasi (unyofu wa nia) ndicho kipimo cha thamani ya amali (matendo)."

Alinukuu pia maneno ya Imam Ridha (a.s) aliyesema:

"Jione kuwa wewe ni mdogo kuliko wengine, kwa sababu huenda wengine wakawa na sifa fulani ambayo wewe huna - na sifa hiyo mbele ya Mwenyezi Mungu ina thamani kubwa."

Ayatollah Ramezani alihitimisha kwa kusema:

"Mtume (s.a.w.w), kwa mtindo wake wa kipekee, aliweka njia ya kuokoa mtu binafsi na jamii. Leo, tunapokaribia miaka 1500 tangu kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu, tunayahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote mafundisho yake."

Na kwa kumalizia, alisisitiza kuwa:

"Maadili si kule kulegeza msimamo, bali ni kufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi kulingana na hali. Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s) ina jukumu la kuitambulisha sira ya Mtume (s.a.w.w) na mafundisho ya AhlulBayt kwa usahihi duniani, na tunapaswa kuzingatia kukuza ujuzi na kutekeleza kwa vitendo mafundisho haya."

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha