19 Septemba 2025 - 17:50
UNIFIL: Israel iache mara moja uvamizi dhidi ya Lebanon

UNIFIL imeitaka jeshi la Israel kusitisha mara moja mashambulizi ya anga dhidi ya Lebanon na kuondoka kabisa kutoka katika ardhi ya Lebanon.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Walinda amani wa Umoja wa Mataifa walioko Lebanon (UNIFIL) wamelaani mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni (Israel) dhidi ya kusini mwa Lebanon, na wametoa wito kwa jeshi la Israel kusitisha mara moja mashambulizi ya anga zaidi.

Katika taarifa yao rasmi, UNIFIL imesema kuwa: “Mashambulizi ya anga ya Israel ya usiku uliopita katika maeneo ya kusini mwa Lebanon ni ukiukaji wa wazi wa Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1701, na ni tishio la moja kwa moja kwa uthabiti dhaifu uliopatikana tangu Novemba mwaka jana. Vitendo hivyo pia vinadhoofisha imani ya raia katika uwezekano wa kufikia suluhisho la amani katika mzozo huu.”

UNIFIL yaendelea kusaidia utekelezaji wa Azimio 1701

UNIFIL iliongeza kuwa: Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kusaidia pande zote mbili (Israel na Lebanon) katika utekelezaji wa Azimio la 1701, wakati huo huo wakiendelea na kazi yao ya kila siku pamoja na jeshi la Lebanon ili kudumisha utulivu kusini mwa Lebanon, hasa katika maeneo ya "mstari wa bluu" (Blue Line) — mpaka wa muda kati ya Israel na Lebanon.

Hatari kwa askari na raia wa kawaida

Katika taarifa hiyo, UNIFIL ilibainisha kuwa: Vikosi vyao vililazimika kuhamishwa kutoka maeneo mawili katika eneo la Deir Kifa, karibu na mji wa Burj Qallawiyah, kutokana na mashambulizi hayo ambayo yaliweka maisha ya askari wa Lebanon, wanajeshi wa UNIFIL, na raia wa kawaida katika hatari kubwa.

Matakwa kwa Israel na pande zote

UNIFIL imetoa wito kwa jeshi la Israel:

1- Kusitisha mara moja mashambulizi ya anga dhidi ya Lebanon

2- Kuondoka kikamilifu kutoka kwenye ardhi ya Lebanon

Pia imesisitiza:“Pande zote lazima zijiepushe na hatua yoyote ya uchochezi au ukiukaji wowote wa makubaliano, ambao unaweza kuongeza mivutano.”

UNIFIL imekumbusha kwamba: “Azimio la 1701 na makubaliano ya kusitisha vita yalitungwa ili kutatua migogoro kwa njia ya amani na kuzuia matumizi ya nguvu au mashambulizi ya upande mmoja.”

Onyo kuhusu kuongezeka kwa mvutano

UNIFIL ilitoa onyo kuwa: “Kuendelea kwa mivutano kunaweza kutishia mafanikio yote yaliyopatikana katika juhudi za kurejesha utulivu.”

Maeneo yaliyoathiriwa na mashambulizi ya Israel

Mashambulizi ya hivi karibuni ya anga ya Israel yamelenga maeneo ya makaazi ya watu katika:

1- Mais al-Jabal

2- Burj Qallawiyah

3- Kafr Tibnit

4- Dibbin

5- Shuhaybah
Maeneo yote hayo yapo kusini mwa Lebanon. Nyumba ziliharibiwa kabisa, lakini wakazi walikuwa tayari wamezikimbia kabla ya Mashambulizi.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha