Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Dkt. Masoud Pezeshkian, siku ya Jumatano tarehe (24 Agosti 2025), katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, alisema: Katika ulinzi wa siku kumi na mbili, wananchi wa Iran wenye mapenzi ya taifa na mashujaa, waliwaonesha wavamizi majivuno yao ya kufikirika. Maadui wa Iran, bila kutarajia, walilitia nguvu umoja mtakatifu wa kitaifa. Wananchi wa Iran, licha ya vikwazo vya kiuchumi vikali zaidi, vya muda mrefu na vizito zaidi, vita vya kisaikolojia na vya kimitandao, na juhudi endelevu za kuleta mgawanyiko, mara tu risasi ya kwanza ilipofyatuliwa katika ardhi yao, walijipanga kwa umoja kumuunga mkono jeshi lao shujaa; na leo pia wanaheshimu damu ya mashahidi wao.
Sehemu ya Hotuba ya Rais wa Iran katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
"Kauli ya msingi ya dini zote na hata dhamiri ya kibinadamu ni kanuni hii ya dhahabu: Usimtendee mwenzako jambo usilolipenda kwako. Nabii Isa (a.s) alisema: Fanyieni wengine vile mnavyopenda kufanyiwa. Mtume wa Uislamu (s.a.w) alisema: Hakuna mmoja wenu anayeweza kuwa muumini kamili mpaka atakapo mtakia mwenzake lile analolitakia nafsi yake.
Hata hivyo, dunia yetu leo imekuwa shahidi wa:
- Mauaji ya halaiki huko Gaza.
- Uvunjaji wa mara kwa mara wa mamlaka na mipaka ya Lebanon.
- Uharibifu wa miundombinu ya Syria.
- Mashambulizi dhidi ya watu wa Yemen.
- Njaa ya kulazimishwa kwa watoto wanyonge.
- Mashambulizi ya kiharamia dhidi ya viongozi wa nchi huru.
Pezeshkian aliongeza: Je, haya mnayoyatenda mngeyapenda kwa nafsi zenu? Ni nani kweli mkiukaji wa amani na usalama wa kimataifa?
Alikumbusha kwamba Juni iliyopita, Iran ilishambuliwa kinyama na Marekani na utawala wa Kizayuni kupitia mashambulio ya anga, hata wakati nchi hiyo ilikuwa njiani kwenye mazungumzo ya kidiplomasia. Alisema: Hili lilikuwa ni pigo kubwa kwa diplomasia, amani na uaminifu wa kimataifa.
Rais wa Iran alisisitiza: Wale wanaotenda jinai hizi wajue kwamba Iran daima imesimama imara mbele ya dhoruba za historia. Wana-Iran, licha ya vikwazo na mateso, walikaa pamoja kwa mshikamano wa kitaifa na leo wanasimama kwa heshima na heshima kuu.
Aidha, alikosoa waziwazi mipango ya "Israeli Kubwa" akisema: Ni mpango wa kiupumbavu na wa kijivuno, unaothibitisha nia halisi za utawala wa Kizayuni ambazo ni za uvamizi na upanuzi wa ardhi.
Pezeshkian alisema: Tunataka Iran yenye nguvu, pamoja na majirani wenye nguvu, katika eneo imara na lenye mustakabali wa matumaini. Tunataka amani inayotokana na nguvu za mshikamano wa pamoja, siyo amani bandia inayotokana na mabavu.
Alikumbusha pia: Kwa miaka mingi, Iran imekuwa miongoni mwa watetezi wakubwa wa eneo lisilo na silaha za maangamizi, lakini mataifa yenye maghala makubwa ya nyuklia ndiyo yanayoshutumu wengine bila haki.
Rais wa Iran alikiri wazi: Iran haijawahi na haitakuwa kamwe katika mchakato wa kutengeneza bomu la nyuklia.
Katika kumalizia hotuba yake, Pezeshkian alinukuu shairi mashuhuri la Saadi:
Binadamu wote ni viungo vya mwili mmoja;
Viungo hivi vimeumbwa kutoka kwa kiini kimoja;
Ikiwa kiungo kimoja kitaumwa,
Viungo vingine haviwezi kupata utulivu;
Wewe usiyesikitika kwa mateso ya wengine,
Si sahihi hata kuitwa mwanadamu.
Kisha akasisitiza: Wahalifu wanaojidai kwa kuua watoto, hawastahili kuitwa binadamu. Iran, kwa msimamo wake wa kiutu na upendo wa kindugu, daima itakuwa mshirika wa kuaminika kwa mataifa yote yanayopenda amani.
Your Comment