Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kumekuwepo na upotoshaji mkubwa unaolenga kuonyesha kuwa Waislamu wa madhehebu ya Shia wanawatusi Masahaba wa Mtume Muhammad (s.a.w.w). Hata hivyo, ukweli ni kwamba Shia hawatukani bali hukosoa kwa hoja na dalili, wakifuata manhaj wa Qur’an na mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s).
1. Shia na Mtazamo wao kwa Masahaba
Shia hawawatusi Masahaba wa Mtume (s.a.w.w), bali hukosoa matendo au maneno ya baadhi yao pale yanapopingana na mafundisho ya Uislamu na Qur’an Tukufu. Kukosoa kwao si kutokana na chuki, bali ni kutokana na ufuasi wa haki na uchambuzi wa kielimu.
2. Qur’an na Mafundisho ya Kukosoa
Uislamu na Qur’an vimejengwa juu ya misingi ya kukosoa kwa hekima. Qur’an yenyewe imewakosoa watu waliopita - kama baadhi ya Mitume, viongozi au wafuasi wao — pale walipofanya makosa, bila kuwatukana. Kwa hiyo, kukosoa siyo tusi bali ni njia ya kujenga na kuelekeza katika haki.
3. Tofauti Kati ya Kukosoa na Kutukana
Akili timamu inatofautisha wazi kati ya kukosoa na kutukana. Kukosoa ni kueleza kosa au upungufu kwa hoja na dalili, huku kutukana ni kutumia maneno ya dharau. Shia wanachagua njia ya kwanza — ya hoja, si ya jazba.
4. Shia na Mafunzo ya Ahlul-Bayt (a.s)
Wafuasi wa Shia hufuata mafundisho na mwenendo wa Ahlul-Bayt (a.s), ambao kamwe hawakufundisha matusi wala dharau. Kwao kuna bahari ya elimu, hoja, na dalili; njia yao ni ya busara na ufuasi wa njia iliyonyooka — njia ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na kizazi chake kitakasifu.
5. Hoja Badala ya Matusi
Mwenye hazina kubwa ya dalili na hoja za kimantiki hana haja ya kutumia matusi. Mtu anayeshindwa kutoa hoja, ndiye anayekimbilia maneno ya kejeli. Kwa Shia, majadiliano ni ya kielimu na kihoja, si ya jazba wala hasira.
6. Qur’an Inasifu na Kukosoa kwa Matendo
Qur’an inawasifu watu kwa matendo yao mema na inawakosoa kwa matendo yao mabaya. Hivyo, inapokosoa watu, haimaanishi kuwatukana. Vilevile, kukosoa baadhi ya Masahaba kwa matendo yao si tusi, bali ni kufuata mfumo wa Qur’an yenyewe.
Your Comment