Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Kikundi cha wanafunzi wa vyuo vya kidini kutoka Iran, Niger, Mali, Lebanon na Iraq walimtembelea Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN), nyumbani kwake jijini Abuja, ambapo walifanya mazungumzo naye kuhusu masuala ya kielimu na kijamii.
Umuhimu wa elimu ya kina na wajibu wa kijamii wa wanafunzi wa dini
Mwanzoni mwa kikao hicho, Sheikh Zakzaky aliwakaribisha wanafunzi hao na kueleza kuwa lengo la mkutano huo ni kukumbusha umuhimu wa njia waliyoichagua. Alisema kuwa kujifunza elimu za kidini si jukumu la mtu binafsi tu, bali ni aina ya kujitolea kwa niaba ya umma wa Kiislamu.
Aliwahimiza kuwa na ufahamu wa dhamira hiyo ili wasipoteze hamasa na bidii katika kujifunza.
Elimu ya kina bora kuliko mahubiri ya juu juu
Kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu Nigeria alisisitiza haja ya kurejea kwenye mbinu asilia za ufundishaji, akisema:
“Tusizibe elimu ya dini kwa mahubiri yenye makelele tu. Ni lazima tuketi, tusome vitabu kwa makini kuanzia mwanzo hadi mwisho, tueleze kila neno, na tuzamishe akili zetu kwenye vyanzo vingine kwa uchambuzi wa kina.”
Alikumbusha kuwa lengo la kujifunza ni kufundisha wengine, akiwataja wanazuoni wa kale wa eneo la Hausaland waliokuwa wakijifunza kwa ikhlasi ili waweze kuelimisha jamii zao.
Sheikh Zakzaky aliongeza kuwa:
“Mahubiri yanayoweza kuunganisha jamii ya Waislamu na kuwafanya wawe mwili mmoja ni jambo jema, lakini elimu na malezi ya msingi haviwezi kubadilishwa na chochote.”
Wanafunzi wa Dini wanatakiwa kuwa kama mishumaa inayoiangazia jamii
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Zakzaky alifananisha wanafunzi wa dini na mishumaa inayoungua ili kuwapa wengine nuru, akisema:
“Wanafunzi wanapaswa kuwa tayari kujitolea muda na nguvu zao ili kuendelea kuwasha taa ya elimu katika jamii.”
Onyo kuhusu juhudi za kuhalalisha Maridhiano na Madhalimu
Kiongozi huyo alionya dhidi ya hatari ya kuzoeza au kuhalalisha uhusiano na watawala madhalimu, akibainisha:
“Wapo wanaojaribu kutushawishi tukubaliane na watawala dhalimu. Sijasema kuwa haiwezekani kuishi nao kwa amani, lakini swali ni: chini ya misingi gani? Je, kama wafuasi wao na waliowekwa chini yao? Kamwe!”
Alisisitiza kuwa ushirikiano na watawala ni halali tu pale unapofanywa kutoka msimamo wa heshima na usawa, lakini kukubali kudhalilishwa au kudharauliwa kama umma wa Kiislamu ni jambo lisilokubalika.
Kumbukumbu ya Imam Hussein (a.s) kama kipimo cha heshima na kusimama imara
Sheikh Zakzaky alikumbusha kisa cha kihistoria cha Imam Hussein (a.s) akisema:
“Kama maridhiano na madhalimu yangekuwa jambo jema, basi Imam Hussein (a.s) angekubaliana na Yazid, na kichwa chake kisingetenganishwa na mwili. Hamwezi kudai kuwa mna ufahamu mkubwa wa maslahi ya umma kuliko yeye.”
Uhuru wa fikra na kujifunza kwa kuchagua
Aliwahimiza wanafunzi kuwa na uhuru wa fikra, huku wakichukua elimu kutoka kwa walimu wao wenye utaalamu katika nyanja tofauti.
Akasema: “Jifunze sarufi, fiqhi au usul kutoka kwa mwalimu anayebobea, lakini linda fikra zako, isipokuwa pale mtakapokuwa na mtazamo mmoja. Ni muhimu kujua unajifunza nini, kutoka kwa nani, na kwa lengo gani.”
Mwisho wa mkutano
Mwisho wa mazungumzo, Sheikh Zakzaky alisisitiza tena umuhimu wa wanafunzi wa dini kutambua kwa uwazi wajibu wao wa kielimu na kijamii, na kuendelea kwa bidii katika njia ya elimu, uelimishaji na utetezi wa haki.
Sheikh Zakzaky akionya: “Kama maridhiano na Madhalimu yangekuwa sahihi, basi kwa hakika Imam Hussein (a.s) angekubaliana na Yazid.”
Your Comment