Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Jakarta - Indonesia, Furqan Amini, Katibu Mkuu wa Mtandao wa Uhuru wa Palestina (FPN) nchini Indonesia, ambaye alihudhuria Mkutano wa 8 wa Kimataifa wa Umoja na Mshikamano na Watoto na Vijana wa Kipalestina uliofanyika hivi karibuni mjini Tehran, ameeleza kuwa Iran si tu inaunga mkono Palestina kisiasa, bali pia ipo bega kwa bega na Wapalestina kwa roho na mali katika uwanja wa mapambano.
Amini amesema Iran imefanikiwa kuunda “mfumo wa ikolojia wa muqawama (ukinzani)” unaounganisha mataifa mengi duniani dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Mtandao wa Uhuru wa Palestina - Umoja na Uratibu katika Miji 89 ya Indonesia
Akizungumzia shughuli za FPN, Amini amesema:
“Mtandao huu kwa sasa unafanya kazi katika miji 89 nchini Indonesia na pia katika baadhi ya miji nje ya nchi. Lengo letu kuu ni kuimarisha umoja na mapambano ya ukombozi wa Palestina kupitia uongozi wa pamoja, uratibu thabiti na juhudi zilizo endelevu.”
Amesema hadi sasa, FPN imeendesha warsha saba za mafunzo kwa wanachama, imefanya mijadala ya mtandaoni (webinars) kwa umma, na kampeni za habari ili kuongeza uelewa kuhusu hali ya Palestina.
Aidha, wameandaa mikutano na maandamano ya wananchi, ikiwemo maandamano mbele ya Ubalozi wa Marekani jijini Jakarta kupinga msaada wa kijeshi kwa utawala wa Kizayuni, na mbele ya Ubalozi wa Misri wakitaka kufunguliwa kwa mpaka wa Rafah. Katika matukio haya yote, matawi ya FPN kote nchini Indonesia yameshiriki kwa wakati mmoja.
“Suluhisho la Mataifa Mawili” ni Njia ya Kudanganya na Kuendeleza Uvamizi
Akizungumzia pendekezo la “suluhisho la mataifa mawili” na hali baada ya kusitishwa kwa vita huko Gaza, Amini alionya:
“Ni kweli kwamba usitishaji wa vita umewapa Wapalestina muda wa kupumua, lakini tunapaswa kuwa waangalifu dhidi ya mpango wa kibepari wa Trump. Haiwezekani Marekani - ambayo ni mshirika mkuu katika mauaji ya Wapalestina - kuwa msuluhishi wa haki. Katika mpango wa vipengele 20 wa Trump, hakuna popote palipotajwa uhuru wa Palestina.”
Amini aliongeza:
“Tumejifunza kutokana na historia kwamba suluhisho la mataifa mawili ni mbinu ya kupoteza muda na kuendeleza uvamizi. Mradi fikra ya Kizayuni bado ipo, amani ya kweli haiwezi kupatikana.”
Nafasi ya Iran katika Kusaidia Palestina
Amini alisisitiza kuwa tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, Iran imekuwa mtetezi thabiti zaidi wa Palestina.
“Iran imekuwa ikitoa msaada wa kisiasa, kiroho na kimwili kwa Wapalestina, na kupitia kujenga mfumo wa muqawama, imeunda mhimili wa kimataifa wa kupinga Uzayuni.”
Amini aliongeza kuwa mikutano kama hii ya kimataifa inayoandaliwa Tehran inachangia kuimarisha mshikamano wa kimataifa dhidi ya Uzayuni na ubeberu, na kuunganisha sauti za upinzani kutoka mataifa mbalimbali.
Ujumbe kwa Watu wa Indonesia: Umoja na Msimamo
Amini ametoa wito kwa watu wa Indonesia, akisema:
“Tunahitaji kuuangalia mzozo wa Palestina kwa mtazamo wa kielimu na wa kina, ili tuweze kuunda harakati za kudumu na zenye matokeo. Adui anatumia mgawanyiko kama silaha yake kuu; nasi tunapaswa kuwa wamoja, tusiweke mbele maslahi ya makundi bali maslahi ya umma wa Kiislamu.”
Ameongeza kuwa leo mataifa kama Yemen, Venezuela, Bolivia, Hispania, na mengineyo yamekuwa yakifanya maandamano makubwa ya kuunga mkono Palestina, na akasema:
“Indonesia nayo inapaswa kuwa kielelezo cha umoja na mapambano ya kupinga dhuluma.”
Kauli mbiu ya mtandao huo ni:
“Kutetea Palestina ni kulinda Indonesia.”
Kumbukumbu ya Muhammad al-Durra na Umoja wa Dunia kwa Watoto wa Palestina
Mkutano huu wa Kimataifa wa Umoja na Mshikamano na Watoto na Vijana wa Kipalestina hufanyika kila mwaka kwa kumbukumbu ya Muhammad al-Durra, mtoto wa Kipalestina aliyeuawa na jeshi la Israel mwaka 2000.
Lengo kuu la mkutano huu ni kuonesha mateso ya watoto wa Palestina wanaoishi chini ya uvamizi na ukandamizaji wa muda mrefu.
Katika mkutano wa mwaka huu, wawakilishi kutoka Palestina, Iraq, Afghanistan, Pakistan, Lebanon, Uturuki, Bangladesh, Tunisia, Serbia, Indonesia, Malaysia, na Zimbabwe walihudhuria.
Mkutano huu uliendana na kumbukumbu ya siku za ushindi wa Iran dhidi ya uvamizi wa Israel, vita vilivyoanza tarehe 13 Juni na kumalizika tarehe 24 Juni, vikimalizika kwa kushindwa kwa utawala wa Kizayuni.
Your Comment