Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Ali Shaiban, Waziri wa Afya na Mazingira wa Yemen, amesisitiza kuwa kuendelea kuzimwa na kusitishwa kwa shughuli za Uwanja wa Ndege wa Sana’a ni kitendo cha jinai na dharau ya wazi kwa mikataba yote ya kibinadamu na kimataifa.
Shaiban, katika mazungumzo yake na Shirika la Habari la Saba, alisema kuwa kufungwa kwa Uwanja wa Ndege wa Sana’a - ambao hivi karibuni ulikuwa shabaha ya mashambulizi ya Israel - kumesababisha dawa na bidhaa za tiba zinazohitaji uangalizi maalumu katika uhifadhi na usafirishaji kuwa adimu au kupotea kabisa.
Ameongeza kuwa mzingiro na kufungwa kwa uwanja huo kumewanyima maelfu ya wagonjwa wa Yemen upatikanaji wa dawa muhimu, yakiwemo madawa ya wagonjwa wa kupandikiza figo pamoja na bidhaa za damu.
Shaiban ameyataka Umoja wa Mataifa na taasisi zake kutoupuuza msiba huu unaochukua maisha ya maelfu ya wagonjwa na kuendelea kuhatarisha maisha ya wengine wengi.
Amesisitiza kuwa vikosi vamizi havizingatii kabisa misingi ya kibinadamu na kimaadili, na licha ya mateso makubwa wanayowekewa wananchi wa Yemen kupitia mzingiro mzito, dunia na mashirika ya kimataifa yameendelea kukaa kimya kwa aibu.
Ameeleza kuwa madhara yasiyo ya moja kwa moja ya vita hii ni makubwa mno kuliko yanavyoweza kupimika, kwani haiwezekani kukadiria ukubwa wa athari zinazotokana na kuwanyima watu dawa na huduma za tiba.
Shaiban amesema kuwa kusimamishwa kwa safari za ndege kupitia Uwanja wa Ndege wa Sana’a kumezuia maelfu ya wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, na pia kumesababisha upungufu wa dawa ambazo hutakiwa kusafirishwa kwa njia ya anga.
Mwezi Mei uliopita, Israel ilishambulia njia kuu ya kutua na kupaa ndege ya Uwanja wa Ndege wa Sana’a kwa kurusha makombora manne, na kusababisha shimo kubwa lenye kina cha takribani mita 20. Njia ya dharura pia iliharibiwa kwa makombora manne mengine, na majengo ya kuwasili na kuondoka, pamoja na vifaa vyote vya ndani, yakateketezwa kabisa. Jengo la usimamizi wa huduma za ndege nalo liliharibiwa kikamilifu. Hasara za awali wakati huo zilifikia karibu dola milioni 500.
Mwisho wa mwezi huo huo, mara baada ya uwanja huo kurejeshwa na safari kuanza tena, Israel iliuangamiza tena kwa shambulio lingine.
Your Comment