Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) - ABNA -, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatollah Syed Mojtaba Khamenei, ametoa ujumbe maalumu kwa mnasaba wa kumbukumbu ya miaka 37 tangu kufariki kwa mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ruhollah Khomeini.
Katika ujumbe huo, Kiongozi huyo amesema kuwa kumfahamu na kumtambua Imam Khomeini ni nguzo muhimu ya kuelewa njia na mustakabali wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Alieleza kuwa mafundisho, misimamo na urithi wa Imam Khomeini bado ni mwongozo kwa taifa la Iran katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kisiasa na kijamii.
Aidha, alisisitiza kuwa kufuata njia ya Ali ibn Abi Talib (as) kumekuwa sifa kuu na chanzo cha fahari katika maisha ya viongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, akiongeza kwamba taifa la Iran limeonyesha mwamko mpya kwa kusimama pamoja na Muhimili wa Muqawama dhidi ya dhuluma na ubeberu.
Kiongozi huyo pia alibainisha kuwa kumbukumbu ya tarehe 14 Khordad, siku ya kufariki kwa Imam Khomeini, imegeuzwa kuwa fursa ya kila mwaka kwa wananchi wa Iran kuhuisha ahadi yao kwa mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuendeleza malengo yake.
Mwisho, ametoa wito kwa wananchi wote kuwa macho dhidi ya njama za maadui kwa kudumisha umoja wa kitaifa, kuwa na utambuzi sahihi wa mambo, kulinda mazingira ya kuaminiana na kuepuka kauli au vitendo vinavyoweza kuwanufaisha maadui wa taifa.
Your Comment