14 Juni 2026 - 12:47
Uchambuzi: Kinachoendelea kati ya Iran na Marekani; Makubaliano au Mkakati wa Kusubiri?

Kwa mujibu wa hali halisi ilivyo, kikwazo kikubwa katika mazungumzo kati ya Iran na Marekani si kufikia makubaliano, bali ni ukosefu wa uaminifu na dhamana ya utekelezaji wake. Tehran inasisitiza kuwa haitasaini makubaliano yoyote kwa shinikizo la Washington, bali yale yatakayolinda maslahi yake na usalama wa eneo.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Mazungumzo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani yanaendelea katika mazingira ya tahadhari kubwa na ukosefu wa kuaminiana. 

Ingawa pande zote zinaonyesha kuwa mlango wa diplomasia haujafungwa, Tehran inasisitiza kuwa haitakubali kusaini makubaliano kwa sababu ya shinikizo la Washington, bali pale tu itakapoona maslahi ya taifa lake yamelindwa kikamilifu.

Kwa mujibu wa msimamo unaotolewa na viongozi wa Iran, changamoto kubwa si kufikia makubaliano, bali ni kuhakikisha kuwa makubaliano hayo yanatekelezwa. 

Iran inaamini kuwa Marekani ina historia ya kujiondoa katika makubaliano ya kimataifa, jambo ambalo limeifanya Tehran kutokuwa na imani na dhamira ya Washington.

Aidha, wachambuzi wanaona kuwa Iran inataka makubaliano yoyote yajikite katika kuhakikisha usalama wa eneo lote la Mashariki ya Kati. 

Miongoni mwa mambo yanayotajwa ni kupunguzwa kwa uwepo wa kijeshi wa Marekani karibu na mipaka ya Iran, kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Gaza, pamoja na kukomeshwa kwa operesheni za kijeshi za Israel nchini Lebanon na kuondoka kwa majeshi yake katika maeneo inayoyashikilia kusini mwa Lebanon.

Kwa mtazamo wa Tehran, masharti hayo yanahusiana na usalama wa kikanda na hayawezi kutenganishwa na mazungumzo yoyote ya kisiasa kati ya Iran na Marekani.

Kwa upande mwingine, Iran inaendelea kusisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia kwa matumizi ya amani ni haki yake ya kisheria chini ya mikataba ya kimataifa, na kwamba haki hiyo si suala la kujadiliwa au kuondolewa kupitia makubaliano ya kisiasa.

Pia kwa mujibu wa hali halisi ilivyo ya ukosefu wa uaminifu kati ya pande hizo mbili, kuna uwezekano Iran ikapendelea kuwepo kwa wadhamini wa kimataifa katika makubaliano yake na Marekani, kama vile Urusi na China, ili kuongeza dhamana ya utekelezaji wa makubaliano yoyote yatakayofikiwa.

Kwa ujumla, mkwamo uliopo leo hii hauonekani kuwa unatokana na kushindwa kwa pande hizo kufikia makubaliano ya msingi, bali unatokana na swali kubwa la nani atakayehakikisha kuwa makubaliano hayo yatatekelezwa kikamilifu. 

Hilo ndilo suala linaloendelea kuwa kikwazo kikuu katika mchakato wa mazungumzo kati ya Tehran na Washington.

Imechambuliwa na: Sheikh Taqee Z. Athumani 

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha