27 Juni 2026 - 20:13
Kauli ya Sheikh Naim Qassem: Makubaliano ya Mfumo kati ya Lebanon na Israel ni “Fedheha na Kusaliti Mamlaka ya Taifa”

Katibu Mkuu wa Hezbollah, Sheikh Naim Qassem, amekosoa vikali makubaliano ya mfumo yaliyofikiwa mjini Washington kati ya serikali ya Lebanon na Israel, akiyataja kuwa ni makubaliano ya fedheha yanayokiuka mamlaka ya taifa la Lebanon na kutoa fursa kwa Israel kuendeleza uvamizi wake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sheikh Naim Qassem, ametoa tamko kali akipinga makubaliano ya mfumo kati ya serikali ya Lebanon na Israel, akisema kuwa yanawakilisha kujisalimisha kwa matakwa ya Israel na Marekani pamoja na kuhatarisha mamlaka na uhuru wa Lebanon.
 

Taarifa ya Katibu Mkuu wa Hezbollah, Sheikh Naim Qassem, kuhusu Makubaliano ya Mfumo kati ya Serikali ya Lebanon na Utawala wa Kizayuni wa Israel ni kama ifuatavyo:


1- Uko wapi uaminifu na wajibu wa serikali ya Lebanon kwa wananchi wake na katika kulinda mamlaka ya taifa la Lebanon? Marekani, ambayo ndiyo mlezi wa serikali hiyo, haikuweza kuipatia Lebanon usitishaji wa mapigano. Na ilipowasilishwa fursa kupitia mazungumzo ya Pakistan kati ya Marekani na Iran mnamo Aprili 2026, serikali iliikataa. Hali hiyo ilisababisha Israel kutekeleza "Jumatano Nyeusi", ambapo mamia ya watu waliuawa na kujeruhiwa, wananchi wakatiwa hofu, na uharibifu mkubwa ukasababishwa kupitia mashambulizi zaidi ya mia moja ya anga katika maeneo mbalimbali ya Lebanon, kuanzia mji mkuu, Beirut.


2- Tuliuambia utawala wa Lebanon kwamba mazungumzo ya moja kwa moja ni maridhiano ya bure kwa Israel, kwani ni mikutano ya kulazimishwa kukubali matakwa ya uvamizi na maagizo ya Marekani na Israel kikamilifu. Mnaenda kwenye mazungumzo hayo huku mkiwa na mgawanyiko na zaidi ya nusu ya wananchi wa Lebanon, na kinyume na katiba na sheria zinazoutambua utawala wa Israel kuwa adui na zinazomwadhibu kisheria yeyote anayeshirikiana nao kwa maneno au vitendo. Hamna hata karata moja ya nguvu kwa sababu kwa hiari yenu mmeachana na nguvu ya muqawama na ya wananchi, na mmeuchoma mgongo muqawama kwa kuutangaza kuwa ni nje ya sheria katikati ya vita, tangu siku ya kwanza, kupitia uamuzi mbaya wa serikali wa tarehe 2 Machi, hatua ambayo ilitumikia mradi wa uvamizi wa Israel. Kujaribu kubadilisha maana ya maneno hakutasaidia; matokeo ndiyo kipimo, na hiki ni kusaliti mamlaka ya Lebanon kwa mujibu wa tathmini ya rafiki na adui.


3- Hati ya maelewano kati ya Iran na Marekani iliweka kusitishwa kwa vita dhidi ya Lebanon kuwa kipengele cha kwanza. Wakati Israel ilikataa kutekeleza hilo, Iran ilisimamisha makubaliano hayo na kuendelea kuufunga Mlango wa Hormuz hadi Marekani ilipoishinikiza Israel na kuilazimisha kusitisha mapigano. Kifungu cha kwanza cha hati hiyo kilisema: "Marekani, Iran na washirika wao katika vita vinavyoendelea wanatangaza, kupitia kutiwa saini kwa hati hii ya maelewano, kusitishwa mara moja na kwa kudumu kwa operesheni za kijeshi katika nyanja zote, ikiwa ni pamoja na Lebanon, na wanaahidi kutokuanzisha tena vita au operesheni za kijeshi dhidi ya kila mmoja wao, wala kutishia au kutumia nguvu dhidi ya kila mmoja, pamoja na kuhakikisha usalama wa ardhi na mamlaka ya Lebanon." Mazungumzo ya kufikia makubaliano ya mwisho yanapaswa kukamilika ndani ya siku sitini, kwa mujibu wa kifungu cha tatu cha hati hiyo.
Serikali ya Lebanon ilikataa tena hadi ilipoeleweshwa na wenye busara na washiriki wa hati hiyo kuwa mapigano yatasimamishwa, jambo ambalo serikali yenyewe ilishindwa kulipata. Hili ni kwa manufaa ya Lebanon, na mazungumzo kuhusu kuondoka kwa Israel yako mikononi mwa Lebanon pekee. Huu ni zawadi ya heshima, utukufu na nguvu kutoka Iran yenye msimamo na uvumilivu kwa Lebanon, watu wake na muqawama wake.


4- Ni anguko gani hili la kutisha? Ni kosa gani kubwa hili la kuachia mamlaka ya taifa kwa adui wa Kizayuni? Netanyahu anaridhia kuimarishwa kwa Jeshi la Lebanon katika maeneo mawili ya majaribio, huku Israel ikifuatilia kupelekwa kwa jeshi hilo na hatua za kunyang'anywa silaha kwa muqawama. Kamati ya pande tatu pia inafuatilia matakwa ya Israel. Kipindi hiki cha majaribio kinaweza kuchukua miezi kadhaa, na hakuna hatua nyingine itakayochukuliwa isipokuwa baada ya kupata "cheti cha tabia njema" kutoka kwa Israel na kutekeleza kile ambacho Israel ilishindwa kukipata vitani.


Kama alivyosema Netanyahu: "Israel itabaki katika ukanda wa usalama hadi Hizbullah itakaponyang'anywa silaha zake nchini Lebanon, na wananchi hawataruhusiwa kurejea katika eneo linalokaliwa."


Serikali ya Lebanon kwa kufanya hivyo inahalalisha kuendelea kwa uvamizi kwa miaka mingi, na huenda hata ardhi hizo zikaunganishwa na utawala wa Kizayuni. Haya ni makubaliano ya kuwanyima Walebanon haki ya kurejea katika ardhi yao.


Kuunganisha kuondoka kwa Israel na kunyang'anywa silaha za muqawama katika Lebanon yote ni pendekezo hatari sana ambalo linavuka mistari yote myekundu na kuifanya Lebanon kuwa chombo cha kuchezewa na Israel.


5- Makubaliano ya mfumo yaliyofikiwa Washington ni fedheha, aibu na kujisalimisha kwa mamlaka ya taifa. Makubaliano haya hayana uhalali wowote, na kinachopaswa kutekelezwa ni vipengele vya hati ya maelewano kati ya Iran na Marekani.
Tutafuatilia kwa njia zote zinazowezekana, pamoja na shinikizo za kimataifa na za Kiarabu, ili Israel itekeleze kifungu cha kwanza cha hati hiyo na iondoke nchini Lebanon.


Tunaiambia serikali ya Lebanon: Ni wakati wa kurudi nyuma kutoka katika makosa yenu yanayoiharibu Lebanon. Sisi tuko tayari kushirikiana kwa ajili ya kulinda mamlaka ya Lebanon, kuikomboa ardhi yake, kuwafukuza wavamizi wa Israel, kuwarejesha wafungwa, kuwarudisha wananchi katika makazi yao, kujenga upya nchi na kufikia makubaliano juu ya mkakati wa usalama wa taifa.


Kusitishwa kwa mapigano kusingewezekana bila kujitolea kwa wapiganaji wa muqawama, familia zao na wananchi wa Lebanon. Tutaendelea kuhifadhi amana ya mashahidi, majeruhi, wafungwa na watu wa ardhi hii, na tutaendelea kama muqawama katika medani ya mapambano hadi uvamizi utakapokoma.


Mwenyezi Mungu amesema:
"Tokeni mkiwa wepesi na wazito, na piganeni kwa mali zenu na nafsi zenu katika njia ya Mwenyezi Mungu. Hayo ni bora kwenu ikiwa mnajua." (Surat At-Tawbah: 41).

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha