29 Agosti 2026 - 23:32
Al-Jamaal Islamic Foundation Yampa Pongezi Sheikh Prof. Alhad Mussa Salum kwa Kuchaguliwa Tena Kuongoza JMAT-TAIFA

Taasisi ya Al-Jamaal Islamic Foundation imempongeza Rais wake, Sheikh Prof. Alhad Mussa Salum, kwa kuchaguliwa tena kwa kishindo kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) kwa kipindi kingine cha miaka 10, huku ikimuombea mafanikio katika kuendeleza juhudi za kuimarisha maridhiano, amani na umoja nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA, Viongozi na wanachama wote wa Taasisi ya Al-Jamaal Islamic Foundation wametoa pongezi zao kwa Rais wa taasisi hiyo, Sheikh Prof. Alhad Mussa Salum, kufuatia kuchaguliwa kwake tena kwa kishindo kuiongoza Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) kwa kipindi kingine cha miaka 10.

Katika ujumbe wao wa pongezi, viongozi na wanachama wa Al-Jamaal Islamic Foundation wameeleza kufurahishwa na uchaguzi huo, wakisema kuwa ni ishara ya imani na matumaini yaliyowekwa kwake katika kuendeleza misingi ya maridhiano, amani, umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Taasisi hiyo imesema ina matumaini kuwa chini ya uongozi wa Sheikh Prof. Alhad Mussa Salum, JMAT itaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kujenga jamii yenye mshikamano na kuimarisha amani na utulivu nchini.

Aidha, Al-Jamaal Islamic Foundation imemuombea Sheikh Prof. Alhad Mussa Salum, ikimtaka Mwenyezi Mungu amjaalie kila la kheri na kumpa wepesi katika kutekeleza majukumu yake mapya, hususan katika kuhakikisha kuwa maridhiano na amani vinazidi kuimarika na kujikita katika maisha ya Watanzania wote.

Tunakuombea Allah akujalie kila la kheri na wepesi katika kila jukumu lako la kuhakikisha Maridhiano na Amani ya nchi vinajikita zaidi katika damu za Watanzania,” ilieleza sehemu ya ujumbe huo wa pongezi.

Taasisi hiyo imehitimisha ujumbe wake kwa kumtakia Sheikh Prof. Alhad Mussa Salum mafanikio mema katika kipindi chake kipya cha uongozi, huku ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana katika juhudi za kuimarisha amani, maridhiano na umoja nchini Tanzania.
 

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha