Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-, Suhail Shahin, Balozi wa Taliban nchini Qatar, katika mazungumzo na kituo cha Al Jazeera amesema kuwa Iran na India walidhani kwamba Taliban ni tegemezi wa Pakistan, lakini sasa wamegundua kuwa dhana hiyo si kweli. Shahin alisisitiza kwamba Taliban wanataka kuwa na uhusiano mzuri na Islamabad, lakini uhusiano huo unapaswa kuwa wa pande zote mbili, na kuwahukumu Taliban kwa matatizo ya Pakistan haina faida kwa mtu yeyote.
Aidha, Shahin alisema kuwa Serikali ya Taliban sasa ndio uhalisia wa Afghanistan, na eneo lote la nchi hiyo liko chini ya udhibiti wa Emirate (Imarati) ya Kiislamu.
Balozi wa Taliban aliongeza kuwa nchi za kikanda pia zimetambua ukweli huu na kwa hivyo zinatafuta ushirikiano na Taliban, jambo ambalo anadhani ni mtazamo wa busara na wa kweli.
Katika mazungumzo mengine na kituo cha habari cha Tolo TV cha Afghanistan, Shahin aliweka wazi kwamba kucheleweshwa tena kutambuliwa rasmi kwa Taliban na nchi mbalimbali hakuna msingi wa mantiki.
Inafahamika kuwa tangu Taliban waliporejea madarakani majira ya joto ya mwaka 2021, na licha ya takriban miaka minne ya utawala wao, bado hakuna nchi yoyote iliyowatambua rasmi kama serikali halali ya Afghanistan.
Your Comment