8 Agosti 2025 - 11:45
Maandamano Makubwa ya Wenyeji Lebanon Kupinga Uamuzi wa Serikali wa Kuvunja Silaha za Muqawama

Wananchi wa maeneo mbalimbali ya Lebanon wamefanya maandamano na mikutano ya hadhara kupinga uamuzi wa serikali wa kuhodhi na kuvunja silaha za vikosi vya Muqawama.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Wimbi la maandamano limeongezeka usiku wa leo katika maeneo ya Kusini na Bekaa, Lebanon, kupinga uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa kuhodhi silaha, huku uvamizi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Lebanon ukiendelea.

Katika mji wa Sur, maandamano ya magari na pikipiki yaliandaliwa, yakihudhuriwa na wafuasi wa Hizbullah na Harakati ya Amal, wakiwa wamebeba bendera na picha za Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah (Katibu Mkuu wa zamani wa Hizbullah) na Imam Musa Sadr.

Washiriki walipiga kauli za kupinga serikali ya Lebanon, Marekani na utawala wa Kizayuni, huku milio ya honi za magari na pikipiki ikitawala mitaa.

Katika eneo la Hermel, maandamano kama hayo yaliandaliwa kuunga mkono Muqawama na kupinga uamuzi wa serikali, ambapo waandamanaji walilitaja kuwa ni matusi kwa sera ya ulinzi wa kitaifa ya Lebanon.

Hali kama hiyo ilishuhudiwa pia mjini Nabatieh na vitongoji vyake, ambako kulifanyika mikusanyiko mikubwa ya magari na pikipiki, ikifuatana na nyimbo za kishujaa na kauli za kuunga mkono chaguo la Muqawama.

Kwa kiwango kidogo, barabara kuu ya Riyaq – Baalbek katika eneo la Midan al-Munthir ilifungwa na waandamanaji.

Kukithiri kwa maandamano haya kumekuja baada ya Waziri Mkuu wa Lebanon, Nauf Salam, kutangaza kuwa baraza la mawaziri limeidhinisha malengo yaliyoainishwa katika dibaji ya waraka uliowasilishwa na Marekani kwa ajili ya kudumisha usitishaji wa mapigano. Waraka huo, uliokabidhiwa na mjumbe wa Marekani Tom Brock, unataka kufutwa kwa hatua za kijeshi za makundi yote yasiyo ya serikali, ikiwemo Hizbullah, kote Lebanon, kusini na kaskazini mwa mto Litani.

Brock ameutaja uamuzi wa serikali ya Lebanon kuwa wa kihistoria na wenye ujasiri, akisema ni hatua ya kutekeleza kauli mbiu ya “nchi moja, jeshi moja.”

Hata hivyo, mawaziri kutoka Hizbullah na Harakati ya Amal waliondoka kwenye kikao cha baraza la mawaziri kilichofanyika Ikulu ya Baabda, kupinga msimamo wa serikali wa kuendelea kujadili suala la kuhodhi silaha katika mazingira ambapo uvamizi wa Kizayuni bado unaendelea, wakilitaja kuwa ni kujisalimisha kwa shinikizo la kigeni na kupuuzia vitisho vilivyopo.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha