Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Katika tukio la kusikitisha lililotokea katika kijiji cha Darul Jamma, kaskazini mashariki mwa Nigeria karibu na mpaka wa Cameroon, watu wasiopungua 55 wameuawa, wakiwemo wanajeshi kadhaa, kufuatia shambulio la usiku lililofanywa na watu wenye silaha.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa maafisa wa eneo hilo na wanaharakati wa kijamii, shambulio hilo lilitokea Ijumaa usiku ambapo washambuliaji waliovamia kijiji hicho kwa kutumia pikipiki walifyatua risasi kiholela na kuchoma nyumba za wakaazi.
Eneo hilo lina kambi ya kijeshi pamoja na makazi ya familia ambazo zilihamishwa kutoka katika kambi za wakimbizi wa ndani baada ya kufungwa mapema mwaka huu.
Mmoja wa walionusurika, Malam Bukar, alisema:
"Walivamia kijiji wakipiga mayowe na kuanza kuwashambulia watu kiholela. Tuliporudi asubuhi, miili ya watu ilikuwa imetapakaa kila mahali."
Babagana Ibrahim, kamanda wa wanamgambo wa kijiji wanaosaidia jeshi la Nigeria, alisema idadi ya waliouawa ni 55, lakini mfanyakazi mmoja wa shirika la misaada la kimataifa alisema idadi hiyo inaweza kufikia 64, wengi wao wakiwa ni wakimbizi waliokuwa wamehamishiwa kijijini hapo kutoka kambi ya Bama.
Ripoti za kiusalama zinaeleza kuwa shambulio hilo liliongozwa na Ali Ngulde, kamanda wa ngazi ya juu wa kundi la kigaidi la Boko Haram linalodhibiti maeneo hayo.
Kanda ya kati ya Nigeria pia imekumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa makundi ya kigaidi, na hali ya usalama inaendelea kuzorota licha ya juhudi zinazoendelea za kijeshi na kiusalama. Serikali ya Nigeria inaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa katika kudhibiti ongezeko la ghasia na ugaidi nchini humo.
Your Comment