Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Msafara wa kimataifa wa "Sumuud", ukiwa na takribani meli 50 zisizo za kijeshi, ulianza safari mwishoni mwa Agosti 2025 kutoka bandari ya Barcelona kuelekea Gaza, kwa lengo la kuvunja mzingiro wa baharini unaoendelea wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza. Msafara huu ulikuwa umebeba misaada ya kibinadamu ikiwemo vifaa vya matibabu na bidhaa muhimu kwa ajili ya kuwasaidia Wapalestina milioni 2.4 walioko chini ya mzingiro.
Msafara huo unajumuisha wawakilishi kutoka nchi 44, wakiwemo wanaharakati, wanasheria, na watu mashuhuri kama Greta Thunberg, mwanaharakati wa mazingira kutoka Uswidi, pamoja na wabunge wanne kutoka Italia. Hivi karibuni, msafara huo ulilengwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (droni).
Mashambulizi haya yalitokea katika maji ya kimataifa, kilomita 56 kutoka kisiwa cha Gavdos nchini Ugiriki, yakihusisha kurushwa kwa mabomu ya mshtuko, gesi za kuwasha, na kuvuruga mawasiliano ya meli. Waandaaji wa msafara wameripoti milipuko 12 dhidi ya meli 9, wakiyaita mashambulizi hayo kuwa "jinai za kivita" na ukiukaji wa amri ya muda ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambayo iliamuru Israel kuruhusu misaada kuingia Gaza.
Hatua za Italia
Serikali ya Italia inayoongozwa na Waziri Mkuu Giorgia Meloni, ilijibu mashambulizi hayo kwa kutuma manowari ya kwanza Fasan mnamo Septemba 24, 2025. Waziri wa Ulinzi Guido Crosetto, siku ya Alhamisi alitangaza kuwasili kwa manowari ya pili Alpino karibu na kisiwa cha Krete (Crete), Ugiriki. Manowari hizi zina vifaa vya hali ya juu vya kugundua na kudhibiti droni, na zimetumwa kulinda raia 56 wa Italia waliopo kwenye msafara, na kusaidia katika operesheni za uokoaji iwapo zitahitajika.
Katika hotuba yake bungeni, Crosetto alilaani mashambulizi dhidi ya meli zisizo za kijeshi na kusisitiza:“Hatua yoyote ya kuzingatia sheria za kimataifa haipaswi kushambuliwa. Shambulizi dhidi ya raia wa Italia katika maji ya kimataifa ni suala la usalama wa taifa.”
Alionya pia kuwa Italia haiwezi kuhakikisha usalama wa msafara huo baada ya kuingia katika maji ya eneo la Israel, kwani Israel inalichukulia hilo kama "tendo la uhasama."
Waziri Mkuu Giorgia Meloni, huku akikosoa msafara huo kwa kuuita “hatua isiyo na uwajibikaji,” alipendekeza misaada ishushwe nchini Cyprus na kusambazwa Gaza kupitia Kanisa Katoliki. Alidai kuwa Italia inaweza kufikisha misaada Gaza ndani ya saa chache.
Hatua za Uhispania
Rais wa Serikali ya Uhispania, Pedro Sánchez, akiwa katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa huko New York, alitangaza kutumwa kwa manowari kutoka bandari ya Cartagena kwa ajili ya kulinda msafara wa Sumuud na kusaidia katika uokoaji ikihitajika.
Sánchez alisisitiza:“Uhispania inasisitiza juu ya haki ya watu wake kusafiri kwa usalama katika maji ya kimataifa, na inapinga vikali matumizi ya viwango viwili vya sheria za kimataifa.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania, José Manuel Albares, alitaja mashambulizi ya droni kuwa “hayakubaliki,” na akaeleza kuwa msafara wa Sumuud una malengo ya kibinadamu tu na si tishio kwa taifa lolote. Aliahidi msaada wa kidiplomasia na wa kibalozi kwa wanaharakati wote waliopo kwenye msafara, wakiwemo raia wa Uhispania.
Msimamo wa Israel
Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ilitoa taarifa ikitangaza kuwa haitaruhusu msafara wa Sumuud kuingia katika maji yanayozunguka Gaza, ikilitaja kuwa “tukio la uhasama.” Walipendekeza misaada ishushwe kwenye bandari za mataifa jirani, nje ya Israel, na isafirishwe hadi Gaza.
Baadhi ya viongozi wa serikali ya Israel, hasa kutoka mrengo wa kulia, walidai kuwa wanaharakati wa msafara wanashirikiana na Hamas – madai ambayo waandaaji wa msafara wameyakanusha vikali.
Mwitikio wa Kimataifa
Colombia na Mexico pia zilitangaza wasiwasi wao kuhusu usalama wa raia wao waliopo kwenye msafara. Rais wa Colombia, Gustavo Petro, kupitia jukwaa la kijamii X (zamani Twitter), alitoa wito wa kuhakikisha usalama na upitishaji salama wa msafara huo. Mexico nayo imesema inafanya juhudi kupitia balozi zake katika ukanda wa Mediterania kulinda raia wake.
Nchini Italia, Elly Schlein, kiongozi wa chama cha Democratic Party (PD), alimkosoa Giorgia Meloni na kutaka badala ya kushambulia msafara, serikali imuhoji balozi wa Israel. Alisisitiza kuwa msafara wa Sumuud unawakilisha nchi 44 na una lengo la kibinadamu pekee – kusaidia watu wa Gaza.
Hali ya Sasa
Msafara wa kimataifa wa Sumuud kwa sasa uko katika maji ya kimataifa karibu na kisiwa cha Krete, chini ya ulinzi wa manowari za Italia, na hivi karibuni za Uhispania. Waandaaji wamesema wataendelea na safari yao kuelekea Gaza, ingawa bado hawajajibu rasmi pendekezo la kushusha misaada Cyprus.
Tukio hili linatokea wakati ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 65,400 wameuawa Gaza tangu Oktoba 2023. Utafiti wa hivi karibuni wa Umoja wa Mataifa unaituhumu Israel kwa kuhusika na ujinai wa mauaji ya halaiki (genocide) huko Gaza, na umetaka kuruhusiwa kwa misaada ya kibinadamu kufika eneo hilo haraka iwezekanavyo.
Your Comment