Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- jarida la Marekani “The National Interest” katika makala yake ya uchambuzi limeonesha shaka kuhusu mafanikio ya mpango wa Donald Trump wa kuleta uthabiti wa kudumu katika Ukanda wa Gaza, na limeonya kuwa mpango huo unaweza kuunda mazingira kwa ajili ya kuibuka kwa taasisi au kundi linalofanana na Hezbollah katika eneo hilo.
Jarida hilo likiashiria uwezekano wa kushindwa kwa pande husika kutimiza masharti ya makubaliano, hasa ikizingatiwa kwamba serikali ya Marekani imeelekeza kipaumbele kwenye masuala mengine ya kimataifa, linasema:
"Hali hii inaweza kuwa fursa kwa Harakati ya Hamas kujijenga upya chini ya kifuniko cha taasisi halali ya kisheria, kisha kuimarisha muundo wake wa kijeshi na shirika."
Kulingana na The National Interest, harakati ya Hamas, licha ya kukubali hatua za awali za mpango wa Trump, imepinga vikali kuondoa silaha zake, na katika taarifa baada ya kutangazwa kwa mapumziko ya silaha imesisitiza kuwa:
"Hata hivyo, hatutakabidhi silaha zetu."
Jarida hilo linaonyesha kuwa masuala ya udhibiti wa Ukanda wa Gaza bado ndiyo kikwazo kikuu cha makubaliano yoyote ya baadaye. Ingawa Hamas inadai inaweza kuachana na baadhi ya silaha za shambulio kama vile mitambo ya kupiga makombora, bado inakataa kukabidhi silaha nyepesi zinazotumika kudhibiti ndani na kuwadhibiti wapinzani.
Hivi sasa, Hamas inajaribu kuimarisha tena udhibiti wake kupitia vitengo vya kijeshi vya kundi la mashujaa.
Kwa mtazamo wa mwandishi wa makala, mkakati wa muda mrefu wa Hamas ni kupata uwakilishi rasmi katika mfumo wowote wa serikali ya Palestina ya baadaye; hatua ambayo, kwa kushirikiana na makundi mengine ya Kipalestina, inaweza kumpa Hamas kifuniko cha kisiasa bila kuachana na nguvu zake za kijeshi.
Mwisho wa makala unasema kuwa mpango wa Trump unahusisha pendekezo la kuunda “taasisi ya mpito ya serikali ya muda mfupi yenye asili ya kiufundi na isiyo ya kisiasa,” lakini matokeo ya mwisho yanaweza kufanana na mfano wa Lebanon kabla ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambapo serikali rasmi ilikuwepo sambamba na nguvu huru ya kijeshi kama Hezbollah ambayo ilitumia ushawishi mkubwa nje ya mfumo rasmi wa Serikali.
Your Comment