Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la AhlulBayt (a.s) -ABNA-, Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, amekiri kuwa juhudi za serikali yake kukabiliana na uvamizi wa utawala wa Kizayuni (Israel) hazijazaa matunda.
Licha ya kusisitiza umuhimu wa mazungumzo na Israel, Aoun alionyesha wasiwasi juu ya ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuendelea kwa vitendo vya kijeshi vya Israel dhidi ya Lebanon.
Alisema: “Utawala wa Kizayuni unaendelea na vitendo vya chuki, ukiukaji wa azimio la Umoja wa Mataifa namba 1701, na unaendelea kushikilia ardhi ya Lebanon huku ukikataa kuwarejesha wafungwa wa Kilebanon.”
Aoun aliongeza kuwa, nchi rafiki za Lebanon zimeombwa kuishinikiza Israel kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano, “lakini hadi sasa hakuna matokeo yoyote mazuri yaliyopatikana.”
Wakati huohuo, Naibu Waziri Mkuu wa Lebanon, Tarek Mitri, ameeleza kwamba shinikizo la kimataifa dhidi ya serikali ya Lebanon linaongezeka, likilenga kuilazimisha Hezbollah kuacha silaha zake.
Mitri alisisitiza kwamba Lebanon imekuwa ikiheshimu kwa ukamilifu makubaliano ya kusitisha vitendo vya kijeshi, huku Israel ikiendelea kuyakiuka.
Pia alibainisha kuwa serikali imeiagiza jeshi la Lebanon kuwa na umiliki wa kipekee wa silaha na kupanua udhibiti wake juu ya maeneo yote ya nchi.
Aidha, alikanusha madai ya Israel kwamba Lebanon haitekelezi wajibu wake, akisema kuwa Rais wa Lebanon hajapokea jibu lolote kutoka Israel kuhusu mapendekezo aliyowasilisha kwa ajili ya kuimarisha usitishaji wa mapigano.
Kauli hizi zinaonyesha changamoto kubwa zinazolikabili taifa la Lebanon, likiwa katikati ya vitendo vya kijeshi vya Israel na shinikizo la kimataifa linalolenga kulidhoofisha jeshi la upinzani (Hezbollah) ambalo linachukuliwa kuwa ngome kuu ya muqawama wa Lebanon.
Your Comment