11 Desemba 2025 - 13:41
Jenerali Qassim Soleimani Aliwahi Kutoa Onyo Kuhusu “Ujasusi wa Luna Al-Shibl”

Jarida la Saudia Al-Majalla limedai kwamba Shahidi Qasem Soleimani aliwahi kuwaonya maafisa wa Syria kuhusu Luna Al-Shibl kuwa jasusi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-, jarida hilo kupitia ripoti ndefu iliyoandikwa na Manaf Saad limechapisha maelezo mapya kuhusu safari ya ukuaji wa Luna Al-Shibl - mtangazaji na mshauri wa masuala ya habari aliyekuwa karibu na Rais Bashar Al-Assad — pamoja na mazingira ya kifo chake mnamo Julai 2024 (Tir 1403), na pia kutoweka kwa ndugu yake Mulham Al-Shibl na mume wake mnamo Aprili 2024 (Farvardin 1403), baada ya shambulio la Israel dhidi ya jengo lililohusishwa na ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus.

Ripoti hiyo kwa mara ya kwanza inafichua maudhui ya mazungumzo yanayodaiwa kufanyika kati ya Shahidi Qasem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds, na Ali Mamlouk, Mkuu wa Ofisi ya Usalama wa Taifa ya Syria. Katika mazungumzo hayo, Soleimani alimwelezea Luna Al-Shibl kama “jasusi”.

Wasifu wa Luna Al-Shibl

Luna Al-Shibl alizaliwa tarehe 1 Septemba 1974 huko Damascus, ndani ya familia ya kidruze. Baada ya wazazi wake kutengana, aliishi na mama yake - mfanyakazi wa chama cha Ba’ath - na akawa mwanaharakati katika idara ya skauti wa chama hicho.

Alihitimu shahada ya lugha ya Kifaransa katika Chuo Kikuu cha Damascus na kuanza kazi katika televisheni ya Syria. Mnamo 2003 alijiunga na kituo cha Al-Jazeera, na mwaka 2008 alifunga ndoa na mwandishi habari wa Lebanon, Sami Kleib, na kupata uraia wa Lebanon.

Inakadiriwa kuwa uhusiano wake na Bashar Al-Assad ulianza mwaka 2008. Mwezi Desemba 2011 alitangaza kupitia kituo cha Al-Dunya kwamba aliachia kazi Al-Jazeera mnamo Mei 2010 na kuamua kuiwekea uzoefu wake serikali ya Syria.

Mnamo Februari 2012 aliingia rasmi Ikulu ya Rais, na baada ya kumuweka kando Buthayna Shaaban, alichukua udhibiti wa kitengo cha habari na kuwa karibu na Asma Al-Assad.

Japokuwa aliolewa tena na Ammar Sa’ati mnamo 2016, inasemekana kwamba Maher Al-Assad aliendelea kumzuia kuhudhuria baadhi ya vikao vyake binafsi.

Onyo la Jenerali Qassim Soleimani

Mnamo mwishoni mwa 2019, Shahidi Qasim Soleimani alitoa onyo kali kuhusu Luna. Alinukuliwa akisema:
“Je, inaingia akilini mtu kuacha mshahara wa dola 10,000 na kuja kufanya kazi kwa pauni 500 za Syria? Huyu ni jasusi.”

Utajiri na Madai ya Ushirikiano na Israel

Kwa mujibu wa Al-Majalla, katika miaka ya karibuni Luna Al-Shibl alipata utajiri mkubwa:

1_Kununua mali zenye thamani ya dola milioni 8 huko Dubai,

2_Kufungua mgahawa wa Kirusi mjini Damascus mnamo Juni 2022.

Yeye na ndugu yake Mulham walikuwa wakiweka wazi misimamo yao dhidi ya Iran na Hizbullah, jambo lililoibua madai kuwa walikuwa na uhusiano au ushirikiano na Israel.

Kifo Chake Chenye Utata

Mnamo 2 Julai 2024, Luna alipata ajali ya gari katika barabara ya Dimas. Alijeruhiwa na kufariki tarehe 6 Julai 2024.

Hata hivyo, picha za gari zilionyesha uharibifu mdogo, na mashahidi walidai kwamba gari lililokuwa likiendeshwa kwa makusudi liligonga gari lake, kisha mtu mmoja akampiga kichwani kabla ya kukimbia.

Baada ya kupelekwa hospitali, kifo chake kilitangazwa kupitia taarifa fupi ya Ikulu, na mazishi yakafanywa kwa hadhira ndogo sana.

Jenerali Qassim Soleimani Aliwahi Kutoa Onyo Kuhusu “Ujasusi wa Luna Al-Shibl”

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha