Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Yván Gil Pinto, ametuma ujumbe rasmi wa pongezi kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi, kwa mnasaba wa kuadhimishwa kwa miaka 47 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Katika ujumbe huo, Gil Pinto aliwasilisha pongezi za dhati kutoka kwa serikali na wananchi wa Venezuela kwa taifa la Iran, akisisitiza uhusiano wa kindugu na mshikamano uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Ameeleza kuwa Venezuela inaiona Iran kama mshirika muhimu, na akathibitisha tena dhamira ya nchi yake ya kuendeleza ushirikiano wa pamoja katika nyanja mbalimbali kwa ajili ya kujenga dunia yenye misingi ya mfumo wa pande nyingi (multipolar world), kusimamia haki ya kijamii, na kushikamana na kanuni zinazohakikisha amani na heshima ya mataifa.
Waziri huyo wa Venezuela pia alisisitiza kuwa ushirikiano wa Tehran na Caracas una nafasi muhimu katika kukabiliana na changamoto za kimataifa na kuimarisha sauti ya mataifa huru katika medani ya dunia.
Ujumbe huo unaonesha kuendelea kwa uhusiano wa kirafiki kati ya Iran na Venezuela na dhamira ya pande zote mbili ya kupanua ushirikiano kwa maslahi ya wananchi wao na amani ya kimataifa.
Your Comment