Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Dar es Salaam - Sheikh Dr. Alhad Mussa Salum, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT-TAIFA), amesisitiza kuwa Swaumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni wajibu kwa Waislamu kwa sababu Mwenyezi Mungu ana huruma kubwa zaidi juu yetu.
Akizungumza katika neno lake la kuukaribisha mwezi wa Ramadhan, Sheikh Alhad Salum alisema:
"Pengine ibada ya swaumu inaweza kuonekana ni chungu, kwa sababu unakaa na njaa na kiu, na unaweza kupata maumivu ya hapa na pale. Lakini lengo la Allah (swt) katika kutuletea ibada hii ni kutuponya kiroho na kimwili."
Aliongeza kuwa kufunga kunakuwa Wajibu kwetu kwa sababu ya ile huruma ya Mwenyezi Mungu juu yetu:
"Allah anajua maslahi yetu ya kiroho na kimwili kuliko sisi wenyewe tunavyojua, hivyo kupitia Swaumu anatutakia maslahi mapana. Ni kama vile daktari anayemlazimisha mgonjwa kunywa dawa chungu - lengo si kumuadhibu, bali kumtibu."
Sheikh Dr.Alhad Mussa Salum amesisitiza kuwa ibada hii ya Swaumu itakuwa fursa kwa Waislamu kurekebisha nafsi zao, kuimarisha Imani zao, na kuungana na huruma ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao ya kila siku.

Your Comment