Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) - ABNA- Imepokewa kutoka kwa Muhammad (s.a.w.w) kwamba katika siku za mwisho za mwezi wa Sha‘bani alitoa khutuba maarufu inayojulikana kama Khutuba ya Sha‘baniyyah, akiwatahadharisha na kuwabashiria Waumini kuhusu fadhila za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Katika sehemu ya khutuba hiyo, Mtume (s.a.w.w) alisema:
“Enyi watu! Hakika umekujieni mwezi wa Mwenyezi Mungu ukiwa na baraka, rehema na maghfira. Ni mwezi ulio bora zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu; siku zake ni bora kuliko siku zote, usiku wake ni bora kuliko nyakati zote, na saa zake ni bora kuliko saa zote. Ni mwezi ambao mmealikwa katika karamu ya Mwenyezi Mungu na mmefanywa kuwa miongoni mwa watu wa heshima mbele Yake…”
Na akaongeza:
… دُعاؤُکُم فیهِ مُستَجابٌ فَاسْأَلُوا اللهَ رَبَّکُمْ بِنِیّاتٍ صادِقَةٍ وَ قُلوبٍ طاهِرَةٍ أَنْ یُوَفِّقَکُمْ لِصِیامِهِ وَ تِلاوَةِ کِتابِهِ …
“......(Pumzi zenu ndani yake ni tasbihi, usingizi wenu ni ibada, matendo yenu yanakubaliwa).... na dua zenu ndani yake zinajibiwa, Muombeni Mwenyezi Mungu Mola wenu kwa nia safi na nyoyo takasifu ili akuwafikisheni muweze kuufunga na kusoma Kitabu Chake…”
Khutuba hii inatukumbusha kuwa Ramadhani si tu mwezi wa kufunga, bali ni msimu wa kujisafisha, kurejea kwa Mwenyezi Mungu, kuimarisha uhusiano na Qur’ani, na kuwajali wahitaji.
Ni wajibu wetu kuupokea mwezi huu kwa toba ya kweli, nia safi, na azma ya kujijenga kiroho, ili tuwe miongoni mwa wanaonufaika na rehema na msamaha wake.
Your Comment