Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) – ABNA – Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Kuaga na Kusimamia Mazishi ya Imam Shahidi (r.a), Ali Akbar Pourjamshidian, amesema kuwa hafla ya mazishi ya Imam wa Umma Shahidi (r.a) itafanyika kwa mipango na maelekezo ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumanne, Pourjamshidian alisema kuwa wanatarajia vyombo vya habari kutekeleza wajibu wake kikamilifu katika kuangazia hafla hiyo kubwa na ya kihistoria, ili iwe kumbukumbu na nyaraka muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha, alieleza kuwa kutokana na hali na mazingira yaliyokuwepo nchini, sherehe za mazishi ya Imam Shahidi zilicheleweshwa hadi sasa ili kuwezesha maandalizi ya hafla ya kitaifa na kimataifa yenye hadhi inayostahili.
Katibu huyo aliongeza kuwa, kwa mujibu wa maamuzi ya familia ya Imam Shahidi (r.a) pamoja na maelekezo ya Kiongozi mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatollah Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei, ratiba na maelezo kamili ya hafla hiyo yatatangazwa katika siku zijazo.
Amesisitiza kuwa hafla hiyo itakuwa miongoni mwa matukio makubwa ya kihistoria yatakayobeba ujumbe wa umoja, heshima na kuenzi mchango wa Imam Shahidi (r.a) kwa Umma wa Kiislamu na ulimwengu kwa ujumla.
Your Comment