Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) – ABNA– Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) limetangaza kuwa limefanya operesheni ya awali ya kujibu mashambulizi ya Marekani, likisema kuwa limeyalenga maeneo 85 muhimu ya kijeshi ya Marekani katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Uhusiano wa Umma cha IRGC, hatua hiyo imekuja baada ya kile ilichokiita ukiukaji wa usitishaji wa mapigano na mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi la Marekani dhidi ya baadhi ya vituo vya pwani na maeneo ya kiraia katika mikoa ya Hormozgan na Mahshahr nchini Iran.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa vikosi vya majini na anga vya IRGC vilitekeleza operesheni ya pamoja kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani (droni), vikilenga maeneo mbalimbali ya kijeshi ya Marekani, yakiwemo Bandari ya Salman, eneo la Makao Makuu ya Meli ya Tano ya Marekani nchini Bahrain, pamoja na Kituo cha Anga cha Ali Al Salem nchini Kuwait.
Aidha, IRGC imesema kuwa katika operesheni hiyo ilifanikiwa kuangusha ndege ya Marekani isiyo na rubani aina ya MQ-9 ambayo ilidaiwa kujaribu kuingilia operesheni hiyo.
Your Comment