Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s.) –ABNA– Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limefanya kikao cha dharura leo, Julai 14, 2026, chini ya uongozi wa Kaimu Mufti wa Tanzania ambaye pia ni Naibu Kadhi Mkuu wa Tanzania, Sheikh Ali Khamis Ngeruko.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya kikao hicho, Baraza limeazimia kumsimamisha Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Walid Alhad Omar Kawambwa, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni mienendo inayokiuka misingi ya uongozi wa Baraza.
Kufuatia uamuzi huo, Baraza limemteua Sheikh Abbas Ramadhani, ambaye ni mjumbe wa Baraza la Mashekhe Mkoa wa Dar es Salaam, kuwa Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam hadi hapo maamuzi mengine yatakapotolewa kwa mujibu wa taratibu za BAKWATA.
Hatua hiyo imefikiwa katika kikao maalumu cha dharura cha Baraza la Ulamaa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa kusimamia maadili, nidhamu na misingi ya uongozi ndani ya taasisi hiyo.

Hadi wakati wa kuchapishwa kwa habari hii, hakukuwa na taarifa ya ziada kutoka BAKWATA inayofafanua kwa kina tuhuma zozote zinazotajwa wala taarifa ya upande wa Sheikh Walid Alhad Omar Kawambwa kuhusu uamuzi huo. ABNA itaendelea kufuatilia na kutoa taarifa pindi zitakapopatikana taarifa rasmi zaidi kutoka pande husika.
Your Comment