17 Julai 2026 - 13:48
Kumbukumbu ya Shahidi Sayyid Ali Khamenei | Ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu Ndiyo Siri ya Athari ya Kudumu

Ujumbe huu unaotolewa katika mnasaba wa kumbukumbu ya Shahidi Ali Khamenei unasema hivi kuwa "Ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu ndiyo msingi wa kudumu kwa matendo mema", huku ukisisitiza kwamba athari ya kweli huzaliwa na nia safi ya kumtumikia Allah (swt).

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Ujumbe huu wa kimawaidha,  unalenga moja kwa moja kuhuisha kumbukumbu ya Shahidi Ali Khamenei (ra) na unaweka mkazo juu ya nafasi ya Ikhlasi (kufanya lolote Kwa ajili ya Allah pekee) katika Uislamu, ukieleza kuwa matendo yanayofanywa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu pekee ndiyo yanayodumu na kuacha athari ya milele katika jamii.

Kwa mujibu wa Mafundisho ya Kiislamu, kazi yoyote ya kheri inapofanywa kwa nia ya kumridhisha Allah (swt) na ikhlasi ikawa msingi wake, Mwenyezi Mungu huipa kudumu na kuifanya iwe na athari isiyofutika katika nyoyo za watu.

Uislamu umetufundisha kuwa mtu anapojitenga na maslahi ya kidunia na kuelekeza juhudi zake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, tofauti za kidunia hupoteza uzito wake, huku roho ikijikurubisha zaidi kwa Mola wake.

Aidha, tunafundishwa pia kuwa viongozi wakubwa wa Kiislamu walifundisha kwamba ukubwa wa Mwanadamu haupimwi kwa mali, cheo au umaarufu, bali kwa usafi wa nia, ikhlasi na uaminifu katika kumtumikia Mwenyezi Mungu. 

Kwa msingi huo, mtu mwenye ikhlasi huwa mfano mwema na nuru inayowaongoza wengine hata baada ya kuondoka kwake duniani.

Ni muhimu pia kukumbuka kuwa athari ya kweli huzaliwa na kujitolea kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu bila kutafuta sifa wala maslahi binafsi.

Matendo ya namna hiyo hubarikiwa na Allah (swt), huendelea kuzaa matunda kwa vizazi mbalimbali na kubaki kuwa taa ya uongofu kwa wanaotafuta haki.

Kwa kuhitimisha ujumbe huu wa Mawaidha mema katika kumbukumbu ya Shahidi na Kiongozi wetu Sayyid Ali Khamenei (ra), tunawaombea Dua njema ya kuwatakia rehema wale wote walioishi na kufariki wakiwa na ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu, sambamba na nuru ya matendo yao mema yanayoendelea kuwaongoza watu katika njia ya haki na uongofu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha