Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Katika Khutba ya Swala ya Ijumaa iliyotolewa katika Madrasat Hazrat Zainab (sa), Kigamboni – Tanzania, Sheikh Swaleh Maulid amezungumzia masuala muhimu ya Akhlaq na tabia njema, akieleza mambo yanayoweza kumsaidia mwanadamu kujilinda dhidi ya vishawishi vya Shetani.
Akibeba anuani kuu isemayo “Mambo Muhimu Yanayomzuia Shetani Asiwe na Nafasi kwa Binadamu,” Sheikh Swaleh amesisitiza mambo matano muhimu:
1. Kumkumbuka Mwenyezi Mungu kwa Dhikri
Ameeleza kuwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu humfanya mwanadamu kuwa macho na kutambua vishawishi vya Shetani, hivyo kumsaidia kujiepusha na maovu.
2. Kusimamisha Swala
Sheikh Swaleh amesema Swala ina nafasi muhimu katika kumjenga mwanadamu katika kumtii Mwenyezi Mungu na kujiepusha na vitendo viovu.
3. Kusoma Qur’ani na Kuitafakari
Amesisitiza umuhimu wa kusoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu pamoja na kutafakari mafundisho yake, ili kuyaweka katika maisha ya kila siku.
4. Kuchagua Marafiki Wema
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuchagua marafiki wenye tabia njema, kwa kuwa mazingira na marafiki vinaweza kuwa na mchango katika mwenendo na tabia ya mwanadamu.
5. Kutubu Haraka Baada ya Kukosea
Sheikh Swaleh amewataka Waumini kutokubali kubaki katika dhambi kwa sababu ya kukata tamaa, bali wanapaswa kutubu na kurejea kwa Mwenyezi Mungu mara wanapokosea.
Katika mawaidha yake, Sheikh Swaleh amesisitiza umuhimu wa mwanadamu kujenga uhusiano wake na Mwenyezi Mungu, kuimarisha ibada na kuchagua mazingira yanayomsaidia katika kuishi maisha yenye maadili mema.
Maoni yako