8 Oktoba 2026 - 11:44
Maandamano ya nchi nzima nchini Morocco dhidi ya kuhalalisha uhusiano na utawala wa Kizayuni

Sambamba na juhudi za Morocco za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi na utawala wa Kizayuni, nchi hiyo ya Afrika Kaskazini imeshuhudia maandamano makubwa ya kitaifa na mikusanyiko ya kuunga mkono Palestina. Waandamanaji wanataka mchakato wa kuhalalisha uhusiano na Israel usitishwe na kuitaka Palestina ipewe msaada mkubwa zaidi.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Habari la Ahlul Bayt -ABNA- Shirika la habari la Al-Araby Al-Jadeed limeripoti leo Jumatatu kwamba, katika siku za hivi karibuni, Morocco imeshuhudia maandamano ya kitaifa, ambapo waandamanaji wametaka kusitishwa kwa mchakato wa kuhalalisha uhusiano na Israel na kuimarishwa kwa uungaji mkono kwa Palestina.

Kampeni hiyo ya maandamano ya siku tatu, iliyomalizika Jumapili, iliongozwa na “Jukwaa la Morocco la Kuitetea Palestina na Kupinga Uhalalishaji wa Mahusiano.”

Maandamano hayo yalifanyika kufuatia tangazo lililotolewa New York tarehe 16 Septemba (25 Shahrivar), lililosainiwa na Nasser Bourita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco; Gideon Sa’ar, mwenzake kutoka upande wa Israel; na Mike Waltz, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa tangazo hilo, Morocco na Israel zitaendeleza ofisi zao za uhusiano hadi kufikia hadhi ya balozi na kuteua mabalozi.

Jukwaa la Morocco la Kuutetea Palestina lilisema kuwa lengo la maandamano hayo ni kuvuta uangalifu wa umma kuhusu matumizi ya balozi, makubaliano na mabadilishano ya kiuchumi katika kujaribu kubadilisha taswira ya uvamizi wa Israel katika ardhi za Palestina.

Kundi hilo pia lilitoa wito kwa vyama vya kisiasa, vyama vya wafanyakazi, makundi ya kiraia na mashirika ya kutetea haki za binadamu kote Morocco kuunga mkono Palestina na kupinga juhudi za kuufanya mchakato wa kuhalalisha uhusiano na Israel kuwa jambo la kawaida katika jamii.

Morocco ilihalalisha uhusiano wake na Israel mwezi Desemba 2020, ndani ya mfumo wa “Mikataba ya Ibrahimu” (Abraham Accords) iliyosimamiwa kwa upatanishi wa Marekani. Morocco ilikuwa miongoni mwa nchi nne za Kiarabu—pamoja na Falme za Kiarabu, Bahrain na Sudan—zilizochukua hatua kuelekea kuhalalisha uhusiano na Tel Aviv katika mwaka huo.

Tangu wakati huo, Israel na Morocco zimeendelea kuwa na ofisi za uhusiano mjini Rabat na Tel Aviv. Mpango wa kuzipandisha hadhi ofisi hizo na kuzifanya kuwa balozi unaashiria kuimarika zaidi kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya pande hizo mbili.

Muadh Al-Hajri, mratibu wa kitaifa wa Jukwaa la Morocco la Kuutetea Palestina, alikosoa hatua hiyo ya hivi karibuni pamoja na mipango ya kuhamishia ofisi ya uhusiano ya Israel katika Mtaa wa Mehdi Ben Barka mjini Rabat. Alielezea uchaguzi wa eneo hilo kuwa “hatua ya uchochezi dhidi ya wananchi wa Morocco na dharau kwa kumbukumbu ya shahidi Mehdi Ben Barka.”

Ben Barka alikuwa mmoja wa viongozi mashuhuri waliopinga serikali ya Morocco. Alitoweka mjini Paris mwaka 1965. Mwaka 2018, Ronen Bergman, mwandishi na mwandishi wa habari wa Israel, alitoa madai mapya kuhusu kutoweka kwake katika kitabu chake Rise and Kill First.

Kwa mujibu wa Bergman, ambaye alifanya utafiti na mahojiano na maafisa wa ujasusi wa Israel waliohusika katika kupanga kutekwa kwa Ben Barka, Mossad ilidaiwa kumpata kwa ombi la shirika la ujasusi la Morocco na kusaidia katika kupanga operesheni ya kumuua, ambayo hatimaye ilitekelezwa na maafisa wa Morocco pamoja na polisi wa Ufaransa. Baadaye, kwa mujibu wa madai hayo, Mossad ilihusika katika kuondoa mwili wake.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha