Shirika la Habari la hlul-Bayt (as) -ABNA- Vyanzo Mbalimbali vya Kiislamu vinanukuu maneno haya mazito na maarufu: ❝Wema hauozi, Dhambi haisahauliki, Allah hafi - Yeye ni Shahidi wa yote mnayoyafanya. Fanya utakavyo na upendavyo, Lakini tambua kwamba Utalipwa kwa kile ulichokifanya.❞
Maneno haya ni ukumbusho mzito kwa kila Muumini kwamba matendo yetu - mema au mabaya - hayapotei. Mwenyezi Mungu, Mjuzi wa siri zote, anaona na atamuweka kila mmoja wetu kwenye mizani ya haki.
Maneno haya ni wito wa kutuweka kwenye mstari wa Ucha Mungu, uwajibikaji wa nafsi, na kujiepusha na dhambi kwa kutambua kuwa hakuna kisichojulikana mbele ya Mwenyezi Mungu (swt).
Tanbihi:
Maneno hayo mazito wengine wanasema kuwa yamesemwa na Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w).
Kiujumla maneno hayo yanapatikana katika vitabu vya Hadithi vya Kiislamu, hasa ndani ya muktadha wa mawaidha ya maadili na siasa ya nafsi.
Ninachoweza kukisema hapa ni hiki kwamba: Ingawa haijathibitishwa kama ni sehemu ya Hadithi "Sahihi" kwa mujibu wa vyanzo vya upande wa Madhehebu ya Kisunni kama vile (Sahih al-Bukhari au Muslim), maneno haya yamenukuliwa kwa wingi sana ndani ya vyanzo vya Kidini vya Waislamu wafuasi wa Madhehebu ya Ahlul-Bayt (as) - Shia Ithna Asharia, na pia yamekuwa yakitajwa mara kwa mara na Wanazuoni wa Kiislamu kama mafundisho ya Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Katika baadhi ya matoleo, maneno haya yanahusishwa na Hotuba ya Mtume (s.a.w.w) au Hotuba ya Imam Ali (a.s), ambapo kiuhalia wake ni maneno yenye kubeba ujumbe wa kimantiki na wa kina katika kuhimiza:
1_ Kufanya matendo mema bila kuchoka.
2_ Kuepuka dhambi kwa sababu hazifutiki bila toba.
3_ Kukumbuka kuwa Mwenyezi Mungu Yu Hai na ni Mjuzi wa Kila Kitu.
4_ Na kwamba kila mtu atalipwa kwa mujibu wa matendo yake.
Kwa hiyo, chanzo chake halisi kinawezekana kabisa kuwa ni:
a) Mafundisho yaliyopokelewa (riwaya) katika vitabu vya Hadithi vya Ahlul Bayt (a.s).
b) Au Hotuba za Mawaidha za Imam Ali (a.s) ambazo nyingi zimekusanywa katika Kitabu Mashuhuri: Nahjul-Balagha.
Your Comment