Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kwa masikitiko makubwa, aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kongwa, Mhe. Job Yustino Ndugai, amefariki dunia leo (tarehe 6 Agosti 2025), akiwa mjini Dodoma.
Taarifa ya kifo chake imetolewa ikieleza kuwa taifa limepoteza mmoja wa viongozi wake wa juu aliyetoa mchango mkubwa katika uendeshaji wa Bunge na maendeleo ya demokrasia nchini.
Mhe. Ndugai, ambaye alihudumu kama Spika wa Bunge kwa vipindi viwili mfululizo, alikuwa pia miongoni mwa wanasiasa waliowahi kushika nafasi mbalimbali muhimu ndani ya chama tawala, na alikuwa maarufu kwa msimamo wake wa kutetea nidhamu na uwajibikaji ndani ya Bunge.
Katika salamu za rambirambi, pole zimetolewa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge la sasa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, familia ya marehemu, wananchi wa Jimbo la Kongwa, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa ujumla.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi. Ameen.
Your Comment