Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Misri sambamba na kuongezeka kwa mashambulizi ya kijeshi ya Israel huko Gaza, imeimarisha vikosi vyake katika kaskazini mwa Sinai, karibu na mpaka wa Gaza na Israel.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Redio na Televisheni la Kizayuni, hatua hiyo ya kuimarisha vikosi vya Misri imechukuliwa kwa ajili ya hali ya tahadhari ya operesheni ya Israel iitwayo “Magari ya Gideoni 2” katika siku za hivi karibuni, kwani Cairo ina hofu kuwa wakazi wa Gaza, chini ya shinikizo la vita vinavyopanuka, watajaribu kuingia katika ardhi ya Misri.
Ripoti hiyo imedai kuwa kuimarishwa huku kunajumuisha kutumwa kwa takribani wanajeshi 40,000 wa Kimasri pamoja na magari ya kivita katika kaskazini mwa Sinai.
Shirika hilo la habari la Kizayuni limeashiria kwamba kiambatanisho cha kiusalama cha mkataba wa amani kati ya Misri na Israel kinasema wazi kuwa kila mabadiliko ya usambazaji wa vikosi karibu na mpaka lazima yaratibiwe na upande mwingine.
Ripoti hiyo ikaongeza kwamba hata kabla ya jeshi la Israel kudhibiti korido ya Filadelfia (iliyo karibu na mpaka wa Misri ndani ya Gaza), Wamisri walikuwa tayari wameonyesha wasiwasi wao kuhusu uwezekano wa wakazi wengi wa Gaza kujaribu kuingia nchini Misri.
Shirika hilo likaendelea kusema kuwa sasa, kwa mtazamo wa Wamisri, hali ya Gaza inaweza kusababisha machafuko karibu na mpaka.
Vyombo vya habari vya Israel, vikimnukuu msemaji wa jeshi la utawala huo, vilisema kwamba “kwa mujibu wa kiambatanisho cha kijeshi cha mkataba wa amani na Misri, kuingizwa kwa vifaa vyovyote vya kijeshi katika Jangwa la Sinai lazima kuratibiwe na jeshi la Israel pamoja na uongozi wa kisiasa.”
Jeshi la Israel Jumatano liliidhinisha kutoa takribani amri 60,000 za kuwaita wanajeshi wa akiba, kama sehemu ya maandalizi ya hatua ya pili ya operesheni “Magari ya Gideoni” itakayotekelezwa huko Gaza.
Misri ina wasiwasi kuwa hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kuenea kwa vita katika eneo hilo inaweza kulazimisha wakazi wa Gaza kuvunja mpaka na kukimbilia nchini Misri, hasa kutokana na kuhamishwa kwa lazima kwa wakazi kuelekea kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Misri mara kadhaa imesisitiza kwamba haitaruhusu uhamishaji wa lazima wa wakazi wa Gaza wala kulifanya eneo hilo lisilokaliwa na watu na hivyo kulazimisha wenyeji wake kukimbia.
Kuhusiana na hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty, alisema kuwa uhamishaji wa lazima wa Wapalestina ni “mstari mwekundu” ambao Misri haitaruhusu uvukwe.
Your Comment