Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kwa lengo la kuimarisha umoja, kueneza elimu ya dini na kuwatia nguvu waumini wa Kiislamu katika maeneo mbalimbali ya nchi, Maulana Sheikh Hemed Jalala ameendelea na Ziara yake ya Kidini katika mikoa kadhaa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiambatana na jopo la viongozi wa Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania (T.I.C).
Ziara hii, ambayo imekuwa ya aina yake na yenye mafanikio makubwa, inalenga kuwafikia waumini katika ngazi za chini, kusikiliza changamoto zao, kutoa mawaidha na kuimarisha shughuli za tabligh na malezi ya kiroho kwa jamii.
Katika moja ya sehemu za ziara yake, Maulana Sheikh Hemed Jalala alitembelea Mkoa wa Kigoma, ambapo alipokelewa kwa mapokezi mazuri kutoka kwa waumini na viongozi wa dini wa eneo hilo.
Moja ya matukio muhimu katika ziara hiyo ni kukutana kwake na Sheikh wa Mkoa wa Kigoma (BAKWATA), Samahat Sheikh Hassan Kiburwa, katika ofisi za BAKWATA Mkoa wa Kigoma, ambapo viongozi hao wawili walifanya mazungumzo ya kina kuhusu maendeleo ya Uislamu, umoja wa Waislamu, na namna bora ya kuimarisha harakati za kidini nchini.
Mazungumzo hayo yalijikita katika kuhimiza ushirikiano kati ya taasisi za Kiislamu, uboreshaji wa elimu ya dini, malezi ya vijana, na kueneza ujumbe wa amani na maadili mema kama msingi wa jamii ya Kiislamu.
Aidha, katika ziara hiyo, Sheikh Jalala aliambatana na msafara wa Tabligh za Mikoani, ambao unaratibiwa na T.I.C na unaongozwa naye mwenyewe. Msafara huo umekuwa sehemu muhimu ya kuhamasisha wananchi kuhusu nafasi ya dini katika kujenga jamii yenye maadili, umoja na uadilifu.
Katika hotuba zake, Maulana Sheikh Hemed Jalala amekuwa akisisitiza juu ya wajibu wa kila Muislamu kulinda umoja, kushikamana na mafundisho ya Qur’an na Ahlul-Bayt (a.s), na kutenda mema kama njia ya kufikia radhi za Mwenyezi Mungu.
Hadithi:
Mtume Muhammad (s.a.w.w.) amesema:
"الْمُؤْمِنُ لِلْمُؤْمِنِ كَالْبُنْيَانِ يَشُدُّ بَعْضُهُ بَعْضاً"
“Muumini kwa muumini mwenzake ni kama jengo; sehemu moja inatia nguvu nyingine.”
Aya Tukufu:
«وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا»
(Surat Aal Imran, Aya 103)
“Shikamaneni nyote kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu, wala msifarakiane.”
Kwa hakika, ziara hii ya Maulana Sheikh Hemed Jalala si tu ishara ya kujitolea kwake kwa ajili ya Uislamu, bali pia ni kielelezo cha uongozi wenye dira, hekima na moyo wa kujenga jamii ya Waislamu iliyo imara na yenye mshikamano wa kweli.
Your Comment