13 Oktoba 2025 - 10:20
Al-Qassam: Makubaliano ya Gaza ni Matunda ya Ustahimilivu - Tupo tayari Kutekeleza Masharti ya Makubaliano Iwapo Mvamizi Israel Atayatii

“Israel ingeweza kuwarejesha mateka wake wengi wakiwa hai miezi mingi iliyopita, lakini ilichagua kupoteza muda na kuendelea na sera ya upumbavu ya kutumia nguvu za kijeshi, jambo lililosababisha vifo vya makumi ya mateka hao mikononi mwa jeshi lake lenyewe.”

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Leo, Tarehe 13/10/2025 - Brigedi za Izz al-Din al-Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Hamas, zimesema kuwa makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni ni matokeo ya ustahimilivu wa wananchi wa Palestina na uthabiti wa wapiganaji wa Muqawamah (upinzani).

Katika taarifa yao rasmi, Brigedi hizo zilitangaza kuwa zitaendelea kuheshimu makubaliano hayo na ratiba zake za utekelezaji endapo tu Israel itatekeleza masharti yaliyowekwa.

Al-Qassam iliongeza kuwa, “Muqawama (mapambano ya Upinzani) daima umekuwa ukijitahidi kusitisha vita vya mauaji ya halaiki, na tulianza juhudi hizo tangu miezi ya mwanzo ya vita; lakini adui alizikwamisha juhudi zote kwa sababu ya maslahi yake finyu na tamaa ya kulisha silika yake ya ukatili na kisasi.”

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa “adui ameshindwa kuwarejesha mateka wake kwa kutumia shinikizo la kijeshi, licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kijasusi na nguvu za kijeshi. Sasa amelazimika kukubali masharti ya makubaliano ya kubadilishana mateka - kama ilivyoahidiwa na muqawama tangu mwanzo.”

Brigedi hizo pia zilisema kwamba “Israel ingeweza kuwarejesha mateka wake wengi wakiwa hai miezi mingi iliyopita, lakini ilichagua kupoteza muda na kuendelea na sera ya upumbavu ya kutumia nguvu za kijeshi, jambo lililosababisha vifo vya makumi ya mateka hao mikononi mwa jeshi lake lenyewe.”

Mwisho wa taarifa, Al-Qassam iliwahutubia wafungwa wa Kipalestina ikisema:
“Gaza na wapiganaji wake wametoa kitu cha thamani zaidi walichonacho kwa ajili ya kuivunja minyororo yenu. Tunaapa kuwa suala lenu litabaki kuwa kipaumbele cha kwanza cha kitaifa mpaka nyote mpate uhuru wenu.”

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha