Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Wanaharakati wa masuala ya utamaduni na dini wamezindua kampeni ya kimataifa inayowaalika Waislamu na watu wa mataifa mbalimbali kushiriki katika usomaji wa Qur’ani Tukufu, dua, tawafu kuzunguka Al-Kaaba Tukufu, na kuzuru maeneo matakatifu kwa lengo la kuhuisha kumbukumbu ya kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah al-Udhma Sayyid Imam Khamenei.
Kampeni hiyo imeanzishwa na International Union of One Ummah, taasisi inayojishughulisha na kuimarisha maelewano baina ya dini mbalimbali, umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu pamoja na shughuli za kimataifa za kibinadamu. Waandalizi wa kampeni hiyo wamechapisha mabango katika lugha mbalimbali ikiwemo Kiingereza, Kiarabu, Kiurdu na Kiazari, wakiwahimiza watu duniani kote kushiriki katika shughuli hizo za kiibada na kiroho.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, kampeni hiyo inalenga kuenzi mchango wa kiongozi huyo kupitia ibada, maombi na matendo ya kiroho yanayosisitiza umoja wa Waislamu na mshikamano wa Umma wa Kiislamu.
Awali, kundi la wanazuoni wa Kishia na Kisunni nchini Iraq lilitoa taarifa maalumu kwa mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, likiwataka kutekeleza ibada ya Hijja kwa niaba ya kiongozi shahidi huyo. Vilevile, wanazuoni wengine wa Kiislamu nchini humo walitoa wito wa kufanyika kwa ibada na dua maalumu ili kuenzi kumbukumbu yake na mchango wake katika Ulimwengu wa Kiislamu.
Your Comment