Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso, Karamoko Jean Marie Traoré, ambaye aliwakilisha nchi yake pamoja na Niger na Mali katika marasimu ya kumuomboleza na kumuenzi Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Sayyid Ali Khamenei (Quds Sirruh), ameeleza kuwa Iran imekuwa mfano wa kipekee wa heshima, uhuru na kujitegemea.
Akikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Abbas Araghchi, Traoré alipongeza ustahimilivu na muqawama wa wananchi wa Iran dhidi ya vitisho na mashinikizo yasiyo halali, akisema msimamo huo umeifanya Iran kuwa kielelezo kwa mataifa mengi yanayotafuta uhuru na mamlaka kamili ya kitaifa.
Katika mkutano huo, Waziri huyo aliwasilisha salamu za rambirambi na mshikamano kutoka kwa Rais wa Burkina Faso, serikali na wananchi wa nchi hiyo, pamoja na wananchi wa Niger na Mali, kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatia kuuawa shahidi kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na idadi ya viongozi pamoja na wananchi wa Iran katika vita walivyolazimishwa.
Aidha, alisisitiza mshikamano wa mataifa hayo matatu ya Afrika Magharibi na Iran katika kipindi hiki cha maombolezo, akieleza matumaini yake kuwa uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya pande hizo utaendelea kuimarika katika nyanja mbalimbali.
Your Comment