Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limedai kuwa katika hatua ya pili ya awamu ya pili ya Operesheni "Nasr 2", limefanya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Kikosi cha Tano cha Wanamaji wa Marekani kilichoko Bahrain.
Katika taarifa yake ya nane iliyotolewa na Ofisi ya Uhusiano wa Umma ya IRGC, jeshi hilo limesema kuwa operesheni hiyo ilitekelezwa kwa kaulimbiu "Ya Litharat al-Husayn (as)", ikiwa ni jibu kwa kile lilichokitaja kuwa uhalifu wa jeshi la Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mashambulizi hayo yalisababisha kuwaka moto kwa matangi ya mafuta ya kikosi hicho na kuharibiwa kwa rada ya ulinzi wa anga ya Patriot, rada ya udhibiti wa anga ya Kikosi cha Tano cha Wanamaji wa Marekani, pamoja na mfumo wa rada wa onyo la mapema wa aina ya C-RAM.
IRGC pia imesema kuwa kituo cha udhibiti na uangalizi wa boti zisizo na rubani kiliharibiwa kabisa, huku ikisisitiza kuwa operesheni zake za kujibu mashambulizi zinaendelea.
Your Comment