Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) –ABNA– Sambamba na maadhimisho ya Sikukuu ya Eid al-Adha, Ukanda wa Gaza kwa mara nyingine umekuwa uwanja wa mashambulizi makali na ya mauti ya jeshi vamizi la Kizayuni. Mashambulizi haya yamelenga maeneo ya makazi ya raia na yamesababisha kuuawa shahidi na kujeruhiwa kwa idadi kadhaa ya watu, wakiwemo watoto na waandishi wa habari.
Miongoni mwa maeneo yaliyoshambuliwa ni kaskazini mwa kambi ya wakimbizi ya Nuseirat na mashariki mwa kambi ya Bureij, katikati mwa Ukanda wa Gaza, ambayo yalilengwa kwa mashambulizi mazito ya mizinga na mashambulizi ya anga.
Kwa mujibu wa vyanzo vya mashinani, jeshi la utawala vamizi wa Kizayuni, mapema leo Ijumaa, limefanya mashambulizi makubwa ya anga katika mtaa wa al-Qarara, kaskazini-mashariki mwa Khan Younis, na kusababisha uharibifu kamili wa nyumba za makazi.
Wakati huohuo, katika mtaa wa at-Tuffah mashariki mwa mji wa Gaza, nyumba kadhaa zimechomwa moto kufuatia mashambulizi ya mizinga. Eneo la Jabal al-Sourani na Jabal ar-Rais pia yamekuwa chini ya mashambulizi mazito ya mizinga.
Mtoto wa Kipalestina, Mus’ab Abu Shawish, pamoja na mama yake, wameuawa shahidi kutokana na mashambulizi ya anga yaliyolenga jengo la makazi karibu na kliniki ya Sheikh Radwan katika mji wa Gaza.
Aidha, Ahmad Qalaja, mwandishi wa habari wa Kipalestina, ameaga dunia kutokana na majeraha aliyoyapata kufuatia mashambulizi ya jeshi la Kizayuni kwenye hema la waandishi wa habari katika hospitali ya Al-Maamadani.
Katika shambulizi jingine, ndege zisizo na rubani za utawala wa Kizayuni zimemuua shahidi mtoto mwingine katika barabara ya ash-Shifa, magharibi mwa mji wa Gaza.
Wakati huu wa Sikukuu ya Eid al-Adha, ndege za kivita na helikopta za Kizayuni zinafanya doria kubwa angani katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza, hasa magharibi mwa Deir al-Balah na kaskazini mwa Khan Younis.
Mwandishi wa Al Jazeera ameripoti kuwa maeneo ya kati na kaskazini mwa Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, yamekuwa yakilengwa kwa mashambulizi ya anga na mizinga.
Your Comment