Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Harakati ya Kiislamu ya Mapambano ya Palestina, Hamas, siku ya Ijumaa ilitangaza kuwa kura ya turufu (veto) ya Marekani dhidi ya azimio kuhusu Gaza ni uthibitisho wa wazi na wa moja kwa moja wa ushirikiano wa Marekani katika uhalifu wa Israel dhidi ya watu wa Palestina walioko Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa rasmi, Hamas ilisema kuwa kutumika kwa kura ya veto na serikali ya Marekani ili kuzuia rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Gaza, ni ishara dhahiri ya kuwa Washington inashiriki kikamilifu katika uhalifu wa Tel Aviv dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
Hamas iliongeza kuwa hatua hiyo ya Marekani ni kutoa mwanga wa kijani kwa Israel kuendelea na mauaji, njaa, na mashambulizi ya kikatili na kihalifu dhidi ya mji wa Gaza.
Katika taarifa hiyo, Hamas ilisema: “Tunawashukuru nchi 10 zilizowasilisha rasimu ya azimio hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na tunazihimiza pamoja na mataifa mengine yote na taasisi za kimataifa kuendelea kuliwekea shinikizo baraza la mawaziri la Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye ni mhalifu wa kivita, ili kusitisha uvamizi huu na kuzuia mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina kuendelea."
Marekani Yapiga Veto Rasimu ya Azimio la Umoja wa Mataifa
Mapema Ijumaa, Marekani kwa mara nyingine tena iliweka kura ya veto dhidi ya rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa iliyolenga kusitisha mauaji ya halaiki ya Gaza, ikiwa ni hatua nyingine ya wazi ya kuunga mkono utawala wa Kizayuni (Israel).
Nchi 10 wanachama wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama walikuwa wamependekeza azimio hilo likisisitiza kusitishwa kwa mapigano kwa kudumu na kutoa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza walioko katika hali ya mateso makubwa.
Mnamo Juni 4, Marekani pia ilipiga kura ya veto dhidi ya rasimu nyingine ya azimio lililokuwa likitaka kusitisha mara moja, bila masharti, na kwa kudumu mapigano kati ya Israel na Hamas, pamoja na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza bila vizuizi.
Your Comment