22 Septemba 2025 - 16:19
Ushinikizi wa Taliban kubadilisha Shule za Kidini kuwa njia pekee ya Elimu kwa Wasichana

Mama mmoja mkoani Nimruz alisema baada ya Mullah kumtaka, alilazimika kuwatoa mabinti zake shuleni na kuwapanga kwenye madarasa ya dini, lakini msaada alioahidiwa haukuwahi kufika. Mama mwingine alisema alipewa masharti: “Ama upeleke binti zako kwenye madarasa ya dini, au hupati chochote.”

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Uchunguzi wa pamoja wa gazeti la The Guardian na tovuti ya Zan Times unaonesha kuwa kundi la Taliban kwa makusudi na kwa mpangilio maalum linajitahidi kubadilisha elimu ya kidini kuwa njia pekee ya masomo kwa wasichana na wanawake wa Afghanistan. Familia zinalazimishwa kwa vitisho na mashinikizo kuwasajili wasichana wao katika shule za dini, au zinahadaiwa kwa ahadi za misaada ya chakula na ajira. Hatua hii kwa hakika inaharibu mustakabali wa kielimu na ajira wa kizazi kipya.

Kwa mujibu wa ripoti ya Guardian, tangu kurejea kwa Taliban madarakani nchini Afghanistan mwezi Agosti 2021, ndoto nyingi za kielimu za wanawake na wasichana zimetoweka. Nahid, msichana mwenye umri wa miaka 24 aliyekuwa akisomea shahada ya Uchumi na alikuwa na ndoto ya kufundisha chuo kikuu, sasa analazimika kutumia asubuhi zake kwenye chumba cha chini ya ardhi mkoani Herat pamoja na wanawake na wasichana wengine 50. Wakiwa wamevaa nguo nyeusi, wanashughulika kusoma na kuhifadhi maandiko ya kidini.

Nahid anasema: “Taliban wanataka kubadilisha fikra za wanawake, lakini mimi nahudhuria tu ili nisiingie kwenye msongo wa mawazo na nipate nafasi ya kutoka nyumbani.” Pia anapokea msaada wa kifedha wa kila mwezi wa takriban 1000 Afghani (sawa na pauni 11), jambo linalompa msukumo mwingine wa kuhudhuria.

Uchunguzi wa Guardian na Zan Times katika mikoa minane umeonesha kuwa Taliban inalazimisha shule za kidini ziwe njia pekee ya elimu kwa wasichana. Baada ya wasichana kunyimwa fursa ya shule za sekondari na vyuo vikuu kwa zaidi ya miaka minne, kundi hili limeunda mtandao mkubwa wa shule za dini.

Ripoti zinaonesha kuwa kufikia mwisho wa mwaka uliopita kulikuwepo zaidi ya shule za kidini 21,000 nchini Afghanistan. Aidha, kati ya Septemba 2024 hadi Februari 2025, Taliban ilijenga au kuanzisha shule mpya za dini zaidi ya 50 katika mikoa 11.

Shule hizi kwa kawaida huendeshwa na walimu wa dini (Mullah) ndani ya misikiti au majumbani na hupokea mishahara kutoka Wizara ya Elimu ya Taliban. Wizara hiyo pia imewapa vyeti vya kufundisha zaidi ya wahitimu 21,000 wa shule za dini ili wafundishe hata vyuoni, hatua ambayo imewaondoa walimu wenye shahada za vyuo vikuu.

Familia ambazo binti zao wamenyimwa elimu rasmi hulazimishwa kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kuwasajili kwenye shule hizi. Baadhi ya Mullah huahidi msaada wa chakula, huku wengine wakisema waziwazi: “Msipowapeleka mabinti wenu, hamtapata msaada wowote.”

Mama mmoja mkoani Nimruz alisema baada ya Mullah kumtaka, alilazimika kuwatoa mabinti zake shuleni na kuwapanga kwenye madarasa ya dini, lakini msaada alioahidiwa haukuwahi kufika. Mama mwingine alisema alipewa masharti: “Ama upeleke binti zako kwenye madarasa ya dini, au hupati chochote.”

Mwenendo huu unabadilisha taratibu desturi za kijamii. Familia zinazokataa zinakosa misaada ya chakula na ajira na kutengwa, huku familia zinazokubali zikiripoti mabinti zao baada ya muda kurudi nyumbani wakiwa na mtazamo mkali zaidi na hata kuwatuhumu wazazi wao kwa “ukafiri.”

Athari pia zimeonekana kwenye shule za msingi za wasichana. Mwalimu mmoja mkoani Nimruz alisema: “Mwaka jana kila darasa lilikuwa na sehemu nne zenye wanafunzi 40. Sasa kuna sehemu tatu tu na kila moja ina wanafunzi 20–25 pekee.” Wengi wamepelekwa moja kwa moja kwenye shule za dini.

Wakati huohuo, walimu wenye shahada za vyuo vikuu wanafutwa kazi na nafasi zao kujazwa na wahitimu wa shule za dini wasio na elimu ya kutosha. Mkurugenzi wa shule moja mkoani Farah alisema walilazimishwa kuwafukuza walimu watano wenye uzoefu, na mmoja wa waliowekwa badala yao hakuweza hata kusoma vizuri, lakini kwa sababu alikuwa na cheti cha dini na uhusiano mzuri na Taliban, alipewa nafasi hiyo.

Mitaala ya shule za dini ni finyu sana: kuhifadhi Qur’ani, mafunzo ya Taliban kuhusu sheria za kidini, majukumu ya kijinsia, na masharti ya mavazi na mienendo. Hakuna masomo ya kisayansi, hisabati, wala elimu ya kisasa.

Vitabu vya masomo vingi huingizwa kutoka Pakistan na kuchapishwa kwa lugha ya Kipushto, hata katika maeneo yenye watu wengi wanaotumia Kifarsi (Dari). Hali hii inawafanya wanafunzi wengi washindwe kuelewa masomo.

Wachambuzi wanasema hata misaada ya kimataifa imekuwa ikihamishiwa kwenye shule za dini. Mfano mmoja ni vifaa vya masomo vilivyotolewa na UNICEF kwa shule ya serikali, ambavyo vilihamishwa hadi kwa darasa la Mullah na mlezi wa shule alilazimishwa kuviorodhesha kama “vilivyopotea.”

Sera hizi pia zinabadilisha soko la ajira. Watumishi wa serikali wenye uzoefu wa miaka mingi wanaondolewa na nafasi zao kujazwa na vijana waliomaliza shule za dini. Mkoani Nimruz, mwanaharakati wa haki za wanawake alieleza kuwa mfanyakazi wa Idara ya Masuala ya Wanawake mwenye shahada ya kwanza na uzoefu wa miaka 20 alifutwa kazi, na nafasi yake kuchukuliwa na msichana wa miaka 17 mwenye cheti cha shule ya dini.

Matokeo ya mwelekeo huu ni kwamba wasichana wengi sasa hawana tena ndoto za kuwa madaktari au wahandisi. Shule za dini ndizo zimekuwa njia pekee wanayoiona kwa ajili ya ajira ya baadaye.

Kwa Nahid, aliyekuwa mwanafunzi wa Uchumi na sasa ni mwanafunzi wa shule ya dini, hali hii ni yenye uchungu na mkanganyiko. Anasema: “Nikibaki nyumbani, nitaumia kisaikolojia. Nikihudhuria darasani, angalau nakutana na wanawake wengine.” Lakini anachokiona ni elimu finyu tu, ndani ya mfumo wa kiitikadi ambao yeye mwenyewe hakubaliani nao.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha