Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-, Hujjatul Islam wal Muslimin Muhammad Saeed Waezi, ambaye ni mwanachama wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qum, alihutubia mkutano wa wanazuoni na wasomi kutoka nchi mbalimbali za Kiislamu uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Kiislamu na Viwanda cha Gaziantep, nchini Uturuki, ambapo alisisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano kati ya wasomi na viongozi wa kidini wa ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kujenga umma mmoja na kustawisha ustaarabu mpya wa Kiislamu.
Katika hafla ya jioni iliyoandaliwa na rais wa chuo hicho, iliyohudhuriwa na kundi la wanazuoni, wasomi na wabobezi wa Kiislamu, Waezi alichambua changamoto na vikwazo vinavyokwamisha uundaji wa umma mmoja wa Kiislamu.
Akiashiria umuhimu wa muungano wa Umma wa Kiislamu, alisema:
“Ubaguzi wa kimadhehebu na kujikita kupita kiasi katika tofauti ndogo ndogo za kimadhehebu ni miongoni mwa vikwazo vikuu vinavyokwamisha juhudi za kuunda umma mmoja na ustaarabu mpya wa Kiislamu.”
Mwalimu huyo wa Hawza ya Qum alibainisha kuwa Waislamu wa madhehebu mbalimbali wana mambo mengi ya msingi ya pamoja katika fikra, utamaduni na itikadi, ambayo yanaweza kuwa msingi thabiti wa umoja wa kweli na ukaribu zaidi kati ya mataifa na wasomi wa Kiislamu.
Mwisho wa hotuba yake, Hujjatul Islam wal Muslimin Waezi alisisitiza: “Kuimarisha mshikamano na ushirikiano wa kielimu na kiakili kati ya wanazuoni na wasomi ni sharti muhimu kwa kushinda changamoto zilizopo na kufanikisha ndoto kuu ya ustaarabu mpya wa Kiislamu.”
Your Comment