Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa ukimya wa Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kuhusu mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, akisisitiza kuwa mashambulizi hayo yanakiuka wazi sheria za kimataifa na kanuni za Wakala huo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ismail Baghaei, ameukosoa vikali msimamo wa kimya wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi, kuhusu mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.
Baghaei aliuliza: “Yuko wapi Rafael Grossi?”, akisisitiza kuwa mashambulizi na vitisho vinavyorudiwa vya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya amani vya Iran vinawakilisha ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran IRNA, Baghaei aliandika katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa X kwamba mashambulizi na vitisho vya mara kwa mara vya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya amani vya Iran havikiuki tu misingi na masharti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa pamoja na sheria za kimataifa, bali pia vinakiuka maazimio ya Bodi ya Magavana ya IAEA, Mkutano Mkuu wa Wakala huo na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Amesema kuwa hatua hizo zinaonesha kwa msingi chuki kubwa ya Marekani dhidi ya sayansi, elimu, maarifa na maendeleo ya Iran.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa shughuli zote za nyuklia za Iran zimewasilishwa kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kwa mujibu wa majukumu ya Iran chini ya makubaliano ya ulinzi na ukaguzi wa nyuklia.
Aidha, amesema kuwa kile alichokiita “msisitizo wa kupindukia wa Marekani” kuhusu eneo la Kuh-e Kolang - linalojulikana pia kama Mlima wa Shoka - ambako hakuna shughuli zozote za nyuklia, si chochote bali ni kisingizio cha kufanya hujuma na uharibifu.
Baghaei amelaani kuendelea kwa mashambulizi na vitisho vya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya amani vya Iran, huku akiukosoa ukimya wa Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kuhusu mashambulizi hayo.
Akisisitiza ukosoaji wake, msemaji huyo aliuliza:
“Yuko wapi Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa?”
Mwisho, Ismail Baghaei amesisitiza kuwa wananchi wa Iran watasimama kwa nguvu zote kukabiliana na uadui wa Marekani na aina yoyote ya uvamizi dhidi ya mamlaka, uhuru na usalama wa kitaifa wa nchi yao.
Maoni yako