Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Dar es Salaam, Tanzania - Madrasat ya Mabanati ya Hazrat Zainab (sa) imeendelea kushuhudia mafanikio makubwa katika darsa zake za Qur’an Tukufu kupitia Mwalimu wa Qur’an, Sheikh Muhammad Ja'far.
Wanafunzi hawa mabinti wa Kiislamu wanajizatiti kwa bidii katika kujifunza Sayansi mbalimbali za Qur’an Tukufu, huku wakihimizwa kuzihifadhi Aya zake na kuzihuisha ndani ya nyoyo zao. Darsa hizi zinalenga kuwajenga kuwa Kizazi bora cha Mabinti wa Kiislamu walio imarika katika msingi imara wa kiroho na kielimu, kwa namna ya kwamba Qur’an Tukufu ibakie kuwa mwongozo wa maisha yao ya kila siku.
Hilo ni katika misingi ya kauli maarufu isemayo “Qur’an ni Uhai Wetu”, ambapo wanafunzi hawa wanahimizwa kuunganisha Sayansi za Qur’an na maisha ya vitendo, ili kufanikisha malezi ya kiakhlaqi na kijamii yenye manufaa kwa Umma wa Kiislamu.
Wanafunzi hawa wa Kiislamu pia wanafundishwa kutambua kuwa Qur’an katika maisha yetu ni chanzo cha uongofu na mwongozo kamili, kwani ndiyo mfumo Sahihi na salama wa maisha ya mwislamu na Mwanadamu kwa ujumla, na kwamba Qur'an Tukufu inapandikiza ndani ya nafsi ya mtu maadili mema, na kumpa utulivu wa moyo pamoja na amani ya nafsi. Aidha, Qur’an humjalia mtu hekima katika kufanya maamuzi na kukabiliana na changamoto za maisha.
Zaidi ya hayo, Darsa hili la Qur’an Tukufu linawafundisha zaidi kuwa Qur'an ni mshirika na muombezi wa yeyote mwenye kushikamana nayo Siku ya Kiyama, hummulikia njia yake hapa duniani, na humuinua katika ngazi za juu Peponi.
Your Comment