9 Februari 2026 - 18:23
Maadhimisho ya Kuzaliwa kwa Imam Mahdi (AS): Vijana Wakumbushwa Wajibu wa Kuijenga Jamii ya Uadilifu katika Kipindi cha Ghaiba

Katika mnasaba wa maadhimisho ya Kuzaliwa kwa Imam Mahdi (AS), Waislamu wa Shia na Sunni walikusanyika kujadili kuhusu Mwokozi wa Ulimwengu na wajibu wa Waumini katika kipindi cha Ghaiba. Khatibu Sheikh Suleimani Abdully aliwakumbusha vijana juu ya umuhimu wa kumcha Mwenyezi Mungu, kushukuru neema Zake na kujenga tabia njema ili kuandaa jamii yenye utu, uadilifu na iliyoepukana na dhulma na ufisadi.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Katika mnasaba wa Kuzaliwa kwa Imam Mahdi (AS) uliowakusanya Waislamu wa Shia na Sunni ili kujadili kuhusu Mwokozi wa Ulimwengu na wajibu wetu katika kuandaa mazingira bora ya kudhihiri kwake. Mnasaba huo ulikuwa ni fursa ya kukumbushana nafasi ya Waumini katika kipindi cha Ghaiba - yaani kipindi cha kumngoja Imam Mahdi (ATFS).

Katika hafla hiyo, Khatibu Sheikh Suleimani Abdully aliwasilisha mada muhimu akiwakumbusha vijana juu ya wajibu wao katika kipindi cha Ghaiba, ikiwemo kujijenga kimaadili, kumcha Mwenyezi Mungu (SWT) na kuimarisha tabia ya kushukuru neema Zake, ili hatimaye kuijenga jamii yenye utu, uadilifu na iliyojiepusha na dhulma na ufisadi.

Iwapo tunataka kusimama imara dhidi ya ufisadi, basi msingi wake ni kumcha Mwenyezi Mungu (SWT) katika kila hali, pamoja na kumshukuru kwa neema alizotujaalia. Kumcha Allah si maneno tu, bali ni kutekeleza amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake katika maisha ya kila siku.

Shukrani kwa Allah hujenga moyo wa uadilifu na unyenyekevu, humfanya mtu atambue kuwa kila alichonacho ni amana kutoka kwa Muumba. Anapomshukuru Mwenyezi Mungu kwa vitendo, basi hata tamaa, rushwa, dhulma na ubinafsi hupungua, kwa sababu anajua kuwa atahisabiwa kwa kila jambo.

Jamii inayojengwa juu ya kumcha Allah na kushukuru neema Zake huzaa watu waaminifu, wanaopenda haki na kuchukia uovu. Ndipo mapambano dhidi ya ufisadi hayabaki kuwa kauli, bali yanakuwa mwenendo wa maisha unaoanza na mtu mmoja mmoja, kisha kuenea katika familia, taasisi na taifa zima.

Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu katika umbo bora kabisa. Jitazame kama mwanadamu: je, unafanana na mbuzi au kuku? Hapana. Umeumbwa katika sura nzuri, kama anavyosema Allah SWT:


﴿لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ﴾


"Hakika tumemuumba mwanadamu katika umbo lililo bora kabisa".

Kwa hiyo tuna kila sababu ya msingi ya kumshukuru Allah SWT kwa neema nyingi alizotuneemesha. Kama alivyosema katika hotuba yake Sheikh Suleimani Abdully, shukrani hizi zisibaki katika maneno, bali zionekane katika tabia, uaminifu, uadilifu na kupambana na ufisadi katika kila ngazi ya maisha.

Kwa hakika, kumcha Allah na kumshukuru Yeye ndiyo nguzo ya kusimama imara dhidi ya ufisadi na kuijenga jamii yenye heshima, uadilifu na baraka.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha