28 Mei 2026 - 14:48
IRGC Yatangaza Mashambulizi ya Kulipiza Kisasi Dhidi ya Kambi ya Marekani

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) limesema limelenga kambi ya kijeshi ya Marekani baada ya shambulizi lililoripotiwa kufanywa karibu na Uwanja wa Ndege wa Bandar Abbas, likionya kuwa uchokozi wowote dhidi ya Iran utakabiliwa na majibu makali zaidi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) limetangaza kuwa limetekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani, kufuatia kile lilichokitaja kuwa ni shambulizi la anga lililofanywa na Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Bandar Abbas alfajiri ya leo.

Katika taarifa yake, IRGC imesema kuwa Marekani ilitumia makombora ya angani kulenga eneo karibu na uwanja huo wa ndege, jambo ambalo limechukuliwa na Tehran kuwa ni kitendo cha uchokozi wa moja kwa moja dhidi ya usalama wa taifa la Iran.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, saa 4:50 asubuhi, vikosi vya Iran vililenga kambi ya kijeshi ya Marekani ambayo ilidaiwa kutumika kama chanzo cha mashambulizi hayo.

IRGC imeeleza kuwa hatua hiyo ni ujumbe wa wazi kwa Marekani na washirika wake kwamba Iran haitakubali mashambulizi dhidi yake bila kutoa jibu.

“Jibu hili ni onyo kali kwa adui kwamba hatua yoyote ya uchokozi haitabaki bila kujibiwa, na ikiwa itarudiwa, basi majibu yetu yatakuwa makali zaidi na yenye maamuzi makubwa,” sehemu ya taarifa hiyo imeeleza.

Aidha, jeshi hilo limesisitiza kuwa upande ulioanzisha mashambulizi ndio utakaobeba kikamilifu matokeo na athari zote zitakazotokana na kuendelea kwa mvutano huo wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati.

Taarifa hiyo imekuja wakati mvutano kati ya Iran na Marekani ukiendelea kuongezeka, huku kukiwa na hofu ya kuenea kwa mapigano mapya ambayo yanaweza kuhatarisha zaidi usalama na uthabiti wa eneo hilo.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha