Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) – ABNA: Mwenyezi Mungu ametajwa katika Aya ya 11 ya Sura Al-Jumu‘ah kuwa ni “Mbora wa Watoaji wa Riziki.” Riziki ambazo watu hupeana wao kwa wao, ikiwa tunaweza hata kuziita riziki, zimechanganyika na mapungufu mengi;
Kwa sababu riziki hizo zina mipaka na ni za muda mfupi, na hakuna uhakika wa kuendelea kwake katika siku zijazo. Wakati mwingine huambatana na kudai fadhila pamoja na kumsababishia mtu madhara ya kimwili au ya kiroho, na wakati mwingine huambatana na kumdhalilisha mtu au kutarajia alipizwe kwa namna fulani; hali ikiwa tofauti na riziki ya Mwenyezi Mungu, ambayo haina mipaka wala ukomo, hakuna hofu kuhusu mustakabali wake, wala ndani yake hakuna kudai fadhila, madhara wala matarajio ya kulipwa.
Bali, riziki ya Mwenyezi Mungu humfikia mwanadamu tangu pale anapokuwa katika hali ya tone la manii ndani ya tumbo la mama yake, na huendelea hadi dakika ya mwisho ya maisha yake. Hata Siku ya Kiyama, riziki hiyo itakuwepo kwa watu wanaostahiki na wanaostahili, katika kiwango cha juu na bora zaidi.
Baadhi ya wafasiri wamenukuu kisa cha mmoja wa makhalifa wa Baghdad pamoja na Bahlul, ambacho kinaakisi kwa namna nzuri mambo yaliyotajwa hapo juu. Inasimuliwa kwamba:
“Khalifa wa Baghdad alimwambia Bahlul: Njoo nikupangie riziki yako ya kila siku ili usiwe na wasiwasi kuhusu riziki yako! Bahlul akamjibu: Ningelikubali hilo kama kusingekuwa na mapungufu kadhaa katika jambo lako!
Kwanza, wewe hujui ninachohitaji; pili, hujui wakati ninapokihitaji; tatu, hujui kiasi ninachohitaji; na nne, huenda siku moja ukanikasirikia na ukaichukua riziki hiyo kutoka kwangu. Lakini Mungu ambaye ndiye anayenipa riziki hana upungufu wowote kati ya hii; na hata siku ninapofanya dhambi, Yeye haikati riziki yangu!”
Mwenyezi Mungu aliyemuumba mwanadamu kutoka katika kutokuwepo na kumfanya awepo, kwa sababu ya uasi wake hakumfungia mtu mlango wa riziki.
Muombe riziki Yeye, kwani Yeye ndiye Mwenye kutoa, na Yeye ndiye anayetekeleza mambo ya kila mja Wake!
Na ingekuwa vizuri Bahlul angeongeza kauli hii pia:
“Ni nani anayekuhakikishia kwamba kesho bado utakuwa kwenye kiti cha mamlaka na utaweza kunipa mimi au mtu mwingine riziki?”
Tunamalizia maneno haya kwa kauli tukufu ya Amirul-Muuminina Ali (a.s.), ambayo ameianza nayo khutba yake maarufu inayojulikana kama Khutba ya Al-Ashbah:
“Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye kunyima na kujizuia hakumuongezei chochote, wala kutoa na ukarimu hakumpunguzii; kwa kuwa kila mtoaji isipokuwa Yeye hupungua, na kila anayezuilia isipokuwa Yeye analaumiwa. Yeye ndiye Mtoaji wa neema za aina mbalimbali na wa ziada unaorudiwa. Viumbe wote ni wategemezi Wake; Amehakikisha riziki zao, amekadiria chakula chao, na ameonyesha njia ya wale wanaompenda na wanaotafuta yaliyoko Kwake. Yeye si mkarimu zaidi kwa kile anachoombwa kuliko kile ambacho hajaombwa.”
Tanbihi:
(1) Tafsiri ya Ruh al-Bayan, Haqqi Bursawi, Ismail, Dar al-Fikr, Beirut, bila tarehe, juzuu ya 9, uk. 528, Sura Al-Jumu‘ah, Aya ya 11.
(2) Chanzo hicho hicho.
(3) Nahj al-Balagha, Sharif al-Radhi, Muhammad bin Hussein, mhariri: Subhi Saleh, Hijrat, Qom, 1414 AH, chapa ya kwanza, uk. 124, Khutba ya 91, kuhusu sifa za Mwenyezi Mungu.
(4) Payam-e Quran, Makarem Shirazi, Nasir, kwa ushirikiano na kundi la wanazuoni, Dar al-Kutub al-Islamiyyah, Tehran, 1386 Shamsi, chapa ya tisa, juzuu ya 4, uk. 416.
Maoni yako