Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Harakati ya Upinzani wa Kiislamu ya Palestina (Hamas), katika maadhimisho ya mwaka wa kwanza wa kuuawa shahidi kwa Yahya al-Sinwar, aliyekuwa mkuu wa zamani wa ofisi ya kisiasa ya Hamas na kamanda wa vita vya “Dhoruba ya Al-Aqsa”, imetangaza kuwa mwenge wa “Dhoruba ya Al-Aqsa” hautazimika, na damu ya viongozi mashahidi itaendelea kuimarisha njia ya mapambano kwa vizazi vijavyo.
Katika tamko hilo imeelezwa:
“Leo umetimia mwaka mmoja tangu kuuawa shahidi kwa Yahya al-Sinwar, mkuu wa zamani wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, alama ya mapinduzi ya Palestina na kamanda wa ‘Dhoruba ya Al-Aqsa’. Watu wa Palestina na harakati za mapambano wamefanikiwa kupata mafanikio ya kitaifa na makubaliano yaliyoshinda njama zote za adui.”
Hamas iliongeza kusema:
“Katika kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa kuuawa kwa kamanda shujaa na mjahid, Yahya al-Sinwar, tunaiheshimu na kuienzi kwa fahari na heshima maisha yake yenye baraka na njia yake ya mapambano. Tangu ujana wake aliishi katika uwanja wa jihadi, na katika miaka 23 ya kifungo chake, kwa uvumilivu na uthabiti aliwashinda watesi wa Kizayuni. Baada ya kuachiliwa kutoka gerezani, aliendelea na juhudi za maandalizi, uundaji wa mipango na uongozi, hadi alfajiri ya tarehe 7 Oktoba 2023, alipofanikisha siku iliyoitikisa dola la uvamizi, ikapindua miundo yake, na kuangamiza hadithi ya jeshi lisiloshindwa. Hatimaye, akapata shahada akiwa katika mstari wa mbele akipigana bega kwa bega na wapiganaji wenzake.”
Tamko hilo liliendelea:
“Tunasema kwa uthabiti kwamba shahada ya kamanda Yahya al-Sinwar, pamoja na viongozi na wapiganaji wengine waliotutangulia katika njia ya jihadi na uhuru, itazidi kuimarisha nguvu, subira na azma yetu, pamoja na taifa na harakati zetu za mapambano, ili kuendeleza njia yao na kuwa waaminifu kwa damu na kujitolea kwao.”
Hamas ikaongeza:
“Mwenge wa ‘Dhoruba ya Al-Aqsa’ utaendelea kuwaka daima, ukiwatia moyo watu wetu kudumisha haki zao, misingi yao, na umoja wa kitaifa. Moto wake katika mioyo ya taifa letu kubwa hautazimika kamwe, ijapokuwa kujitolea ni kwa gharama kubwa na nguvu za adui ni nyingi. Tunasalia waaminifu kwa agano letu na viongozi mashahidi: Bendera haitadondoka ardhini, bali itaendelea kuinuliwa na kutikisika, ili kila mtoto wa taifa letu aipokee kizazi baada ya kizazi na kuilinda, hadi uhuru kamili na kuundwa kwa dola huru ya Palestina yenye mji mkuu Quds vitakapopatikana.”
Hamas ilisisitiza:
“Katika kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa shahada yako, ewe Abu Ibrahim, pumzika kwa amani; maana umetimiza amana, umejihad katika njia ya Mwenyezi Mungu, umeishusha bendera ya adui, umevunja majivuno yake na kutikisa misingi ya uwepo wake wa uongo. Ingawa mwili wako mtukufu haupo nasi hapa Gaza, roho yako inayoruka angani inadhibiti kuwa damu ya mashahidi inaandika utukufu wa milele wa Palestina na umma. Adui ameshindwa kufikia malengo yake ya uvamizi katika ardhi ya Gaza, na hatimaye amelazimika kukubali kusitisha mapigano, huku wafungwa wake wakirudishwa tu kwa mujibu wa masharti na uamuzi wa mapambano.”
Mwisho wa tamko ulisomeka:
“Rehema, heshima na utukufu wa milele viwe juu ya roho ya kamanda shujaa shahidi Yahya al-Sinwar (Abu Ibrahim), na juu ya misafara yote ya mashahidi miongoni mwa viongozi, watoto wa taifa letu na wa umma wetu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awape makazi yao katika Firdaws al-A‘la, wakiwa pamoja na Mitume, wakweli, mashahidi na wema; na hao ndio wenzi bora kabisa.”
Yahya Ibrahim Hasan al-Sinwar, anayejulikana kwa jina la “Abu Ibrahim”, aliuawa shahidi tarehe 16 Oktoba 2024 (sawa na 25 Mehr 1403 Hijria Shamsia) mikononi mwa wanajeshi wa Kizayuni katika mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Your Comment