Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-, Majlisi ya maombolezo ya Mwezi Mtukufu wa Muharram imefanyika katika Jamiat Al-Mustafa jijini Dar es Salaam, Tanzania, kwa ushiriki wa waumini na wapenzi wa Imam Husayn ibn Ali.
Majlisi hiyo iliongozwa na mhadhiri Sheikh Taqee Zacharia Athumani, ambaye aliwasilisha mada kuu yenye kichwa: "Kwa nini tunahuisha utajo wa matukio ya dhulma dhidi ya Imam Hussein (a.s.), mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.), katika ardhi ya Karbala?"
Katika muhadhara wake, Sheikh Taqee alieleza kuwa kuhuisha kumbukumbu ya Karbala si kwa lengo la kufufua huzuni pekee, bali ni kuhifadhi ukweli wa historia ya Kiislamu, kuendeleza maadili ya kusimama dhidi ya dhulma, na kuwakumbusha Waislamu wajibu wa kutetea haki na uadilifu katika kila zama.
Aidha, alisisitiza kuwa vikao vya maombolezo ya Muharram vinaendeleza ujumbe wa Imam Husayn ibn Ali wa kujitolea kwa ajili ya dini, kupambana na uonevu na kulinda misingi ya Uislamu. Aliongeza kuwa kuikumbuka Karbala ni njia ya kuimarisha uhusiano wa Waumini na Ahlul-Bayt wa Mtume (s.a.w.w.) na kuhamasisha jamii kuishi kwa misingi ya haki, subira na uwajibikaji.
Majlisi hiyo ilihitimishwa kwa dua na maombolezo ya kuwakumbuka mashahidi wa Karbala, huku waumini wakisisitizwa kuendeleza mafunzo ya Ashura katika maisha yao ya kila siku.
Your Comment